Tuesday, 3 March 2009

Upimaji Ardhi TZ

Wananchi waanza kupimiwa ardhi

Serikali imeanza kuchukua hatua ya kurasimisha ardhi na nyumba za wakulima na wafugaji ili kuwawezesha kupata mikopo benki, mifuko na taasisi za fedha nchini ili kuwaondoa katika umaskini uliokithiri.

Kauli hiyo ilitolewa juzi na Waziri wa ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, John Chiligati wakati akizindua upimaji na utoaji wa hati miliki za ardhi kimila uliofanyika Wilaya ya Bariadi mkoani Shinyanga.

Wilaya hiyo ni moja ya maeneo ya majaribio kitaifa. Nyingine ni ya Babati mkoani Arusha pia.

Uzinduzi huo wa mpango umefanyika baada ya viongozi wa serikali na vyama vya kisiasa na wataalamu kupewa mafunzo elekezi wilayani humo ya kuchambua chimbuko la mradi huo katika utekelezaji wa sera ya Taifa ya Ardhi ya mwaka 1995 na Sheria ya Ardhi ya Vijiji namba 5 ya mwaka 2004.

Chiligati alisema hatua hiyo ni ya utekelezaji wa Mkakati wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara Tanzania (Mkurabita) kwa lengo la kuwawezesha Watanzania kurasimisha ardhi na nyumba zao ili waweze kuzitumia kupata mikopo kwa urahisi.

Alisema mpango huo ambao ni wa kwanza kutekelezwa nchini utawawezesha wakulima na wafugaji kumiliki ardhi zao za kimila kwa kuhusisha serikali za vijiji na kupanga matumizi bora ya ardhi.

Alisema maeneo muhimu ambayo yatazingatiwa wakati wa upimaji huo ni ya makazi, huduma za kijamii, makaburi na maeneo ya hifadhi ya ardhi ya kijiji kama vile maeneo ya malisho.

Alisema baada ya kutambua kila kipande cha ardhi ndani ya kijiji chini ya mpango huo, ndipo utekelezaji utafanyika kwa kutambua mipaka ya kila mwenye shamba au eneo la malisho ya mifugo na kuweka mipaka bayana.

Pamoja na kuweka kumbukumbu za miliki ya ardhi bayana, alisema mpango huo pia utammilikisha na kumpatia kila mhusika hatimiliki ya eneo lake, wakati kipande cha ardhi kwa mtu mmoja mmoja au familia ya mume na mke au eneo linalomilikiwa kiukoo itamilikishwa kwa kupitia kiongozi wa familia au ukoo.

Chiligati aliagiza kuwapo kwa ushirikishwaji wa kila mwanakijiji na kuutaja mradi huo kuwa ni shirikishi.



SOURCE: Nipashe, 2009-03-03 10:55:06
Na Stephen Wang`anyi, Shinyanga

No comments:

Post a Comment