Tuesday, 10 March 2009

'Umependa Ua, Boga Lake Je?'

.
.
Anakupenda ukiwa na mumeo, lakini ukiachwa yeye anakutosa

Mpenzi msomaji, wapo watu wengine aibu kwao ni mwiko. Kazi yao ni kama golikipa anayesubiri mpira golini ili audake au auteme kama mambo yakiwa magumu.

Naam. Ipo tabia moja ambayo imekuwepo kwa muda sasa ndani ya jamii yetu na inatesa baadhi ya familia lakini wahusika wanagumia maumivu kimya kimya wasijue cha kufanya.

Eti bila haya wala huruma ya kibinadamu unamendea cha mwenzio na kukorofisha ndoa yake au unyumba wake, lakini bibie akiachwa kwa ajili yako, nawe unamtosa. Ebo!

Tabia hii naweza kuitolea mifano katika sura mbili tofauti. Sura ya kwanza ni wale wanaume mafedhuli, tena wenye ndoa zao wanapodiriki kuwarubuni wake za wenzao na kujenga mahusiano, lakini pindi wenye wake wanapong`amua na kuwaacha, nao pia wanawatosa. Si unajua tena mshika mawili moja humponyoka? Mimi naongezea kuwa mshika mawili pia yote yaweza kumponyoka.

Sura ya pili ni ile mijamaa inayomezea wake za wanaume wenzao na pindi mahusiano hayo yanapogundulika, basi dowezi yule huamua kumchukua mke yule jumla jumla.

Yaani unasubiri mwenzio achague mchuchu wake, achombeze gharama kibao na hata amzalie mtoto au watoto, kisha wewe ujichukulie kiulaini? Hawa hawamuogopi Mungu anayekemea kutotamani cha mwenzako ikiwa ni pamoja na mke? Ama kwa hakika Maisha Ndivyo Yalivyo.

Katika sura ile ya kwanza hebu nikupe mfano mmoja ninaokumbuka uliotokea hapa jijini miaka ya nyuma. Yupo mama mmoja aliyekuwa na ndoa yake imara na alibahatika kuzaa watoto wake wawili.

Mumewe aliheshimu sana ndoa yake na hata kama alikuwa akichepuka kusaka vidosho alifanya kwa siri sana.

Mkewe kwa kuchukulia upole wa mumewe, tamaa zikamfanya avunje uaminifu na katika pilikapilika zake akampata mtaalamu mmoja mzungu aliyekuwa nchini kikazi. Kwa siri mzungu huyu akamjengea nyumba mama huyu.

Aliimarisha mahusiano hayo kwa siri hata akapata ujauzito wa mzungu. Hali hiyo ilimfanya wakati mwingine ajisahau na kutorudi nyumbani. Akiulizwa anatoa sababu zilizotia shaka.

Hata hivyo, akatafuta mazingira ya kumkorofisha mumewe na hapo akatoweka nyumbani kabisa. Mume alipochunguza akagundua kuwa amewekwa kinyumba na mtaalamu huyo wa kizungu.

Ilibidi mume apate ushauri toka kwa washenga, wazee wa koo za pande zote mbili. Mke akaitwa kwenye kikao akakataa. Mume huyu akaamua kuvuta pumzi aone mwisho wa mama huyu.

Ilifikia wakati mzungu yule akamuuliza mwanamama huyu mbona haendi nyumbani kuona familia yake, lakini naye akawa anamvunga kuwa imehamia mikoani ndio sababu yuko naye wakati wote.

Nyumba ikawa imekamilika na mzungu na bibie wakahamia na siku chache baadaye akajifungua mtoto chotara. Mzungu hakutaka azae mtoto na mama yule hasa kwa kutambua kuwa alikuwa mke wa mtu.

Alipoona mtoto mzungu ikabidi atafute mazingira ya kumtoroka bibie.

Siku moja bibie alitoka kwenda kwa jamaa zake na ndipo mzungu akapata mwanya wa kuishia zake. Pengine ni kwa kuhofia kushtakiwa kwa kuvuruga ndoa ya mwanaume mwenzie.

Bibie kurudi akagundua kuwa mzungu alishachukua vitu vyake vyote muhimu na alipochunguza kazini akajibiwa kuwa alishaondoka zake kurudi ulaya.

Mama huyu akabaki ameduwaa asijue la kufanya. Kwa mume hawezi kurudi hasa baada ya kuzaa nje ya ndoa.

Katika sura ya pili, yupo mwanamama mmoja ambaye naye alikuwa na ndoa yake imara huku wakijaliwa kupata watoto watatu. Lakini kwa tamaa zake, akaivunja mwenyewe na sasa yupo yupo tu.

Mumewe alikuwa mtumishi wa umma mwenye madaraka. Walikuwa wamejenga nyumba yao nzuri, watoto wanne na mtoto wao mkubwa tayari amemaliza chuo.

Bibie huyu pamoja na kutunzwa vema huku akiwa na shughuli zake za ujasiriamali, lakini bado aliruhusu mahusiano ya nje na bosi mmoja mwenye cheo serikalini.

Ni bosi mwenye mke na watoto kibao, tena kwa wanawake tofauti. Mahusiano haya yakawa moto.

Wapambe wa mume huyu wakamtaarifu nyendo za mkewe na bosi yule. Mume bila taharuki akachunguza kwa muda.

Hatimaye aliwafuma wakiwa ndani ya gari na alipoulizwa akajitetea kuwa ilikuwa ni lifti.

Hata hivyo, jamaa akatafuta watu wawili ambao walikuwa wakimuona bibie na kibosile yule na kutoa ushahidi, tena mbele ya washenga.

Mume huyu hadi leo hajatoa talaka lakini aliamua kutengena na mkewe na tayari ameshaoa mke mwingine. Bibie naye akaona kuliko akose kote afadhali amuegemee kibosile yule.

Kwa sasa amepangishiwa nyumba na amekuwa mmoja wa wake wadogo wa bosi yule. Swali ni je, vituko vya aina hii vina tija gani katika maisha haya?

Yafaa kinamama na kinababa wajiulize migongano ya aina hii ya kimahusiano yanayobomoa nyumba zao, nini basi kifanyike?

Una mke au mume mzuri ambaye ulimchangua mwenyewe, sasa hizi tamaa za fisi zinatoka wapi? Hata kama utasema chaguo lile halikuwa lako au ulikosema kuchagua, sasa kwanini uopoe wa mwenzio? Huu ni wizi mtupu, tena wa mchana kweupe.

Tabia hii ya kutamani vya wengine imevuruga nyumba zetu nyingi. Yafaa watu wabadilike, hasa kwa kuzingatia` kuwa tabia hii imechangia sana kuenea kwa maambukizi ya virusi vya ukimwi, ongezeko la watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi kutokana na ama wazazi kuachana. Kutengana au hata kufa.

Ulaghai wa baadhi ya kinababa nao siachi kuukemea kwani umechangia baadhi ya kinamama kuhadaika kwa kununuliwa magari, kujengewa nyumba na hata kuanzishiwa miradi ya kibiashara na watu wengine nje ya ndoa zao.

Binafsi naona ni mateso ya kiroho wanayopata wale wote waliojikuta kwenye mtego inayohusiana na mifano niliyotaja na mengineyo.

Zaidi pia ni majuto kwani walioharibu nyumba zao wenyewe, bila shaka wanazitamani tena lakini inashindikana. Si unajua maji yakimwagika hayazoleki?

Naam. Mpenzi msomaji niishie hapa nikupe fursa nawe uchangie ili sote kwa pamoja tuelimishane na jamii yetu kwa jumla. Ukiwa nayo maoni, hata jambo linalokukera kuhusu maisha ndani ya familia zetu, nikandamizie kupitia:

fwingia@yahoo.com
Wasalaam.


SOURCE: Nipashe, 2009-03-08 11:35:45
Na Anti Flora Wingia

No comments:

Post a Comment