Friday, 6 March 2009

Hotuba ya Mhe Rais Kikwete (Jeshini)

HOTUBA YA MHESHIMIWA JAKAYA MRISHO KIKWETE, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA NA AMIRI JESHI MKUU WA JESHI LA ULINZI LA WANANCHI WA TANZANIA, KWENYE UZINDUZI WA KAMANDI YA JESHI LA NCHI KAVU YA JESHI LA ULINZI WA
WANANCHI WA TANZANIA, MSANGANI, PWANI,
TAREHE 04 FEBRUARI, 2009

Mheshimiwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la
Kujenga Taifa;
Mheshimiwa Naibu Waziri wa Elimu na
Mafunzo ya Ufundi;
Mheshimiwa Mkuu wa Majeshi;
Mnadhimu Mkuu wa Jeshi;
Mheshimiwa Katibu Mkuu;
Waheshimiwa Viongozi wa Serikali;
Wakuu wa Majeshi Wastaafu; Wanadhimu Wakuu
Wastaafu na Majenerali Wastaafu
Kamanda Kamandi ya Nchi Kavu;
Ndugu Makamanda na Wapiganaji;
Wageni Waalikwa;
Mabibi na Mabwana.

Napenda kuanza kwa kutoa shukrani zangu za dhati kwa heshima mliyonipa ya kunishirikisha kwenye sherehe hii adhimu ya uzinduzi wa Kamandi ya Jeshi la Nchi Kavu ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania. Kunishirikisha kwenu kwenye tukio hili muhimu kunanipa faraja kubwa kwani nami ninakuwa sehemu muhimu ya historia ya maendeleo ya Jeshi letu.
Waheshimiwa Mawaziri, Makamanda na Wapiganaji;
Siku ya leo ni siku muhimu sana katika historia ya jeshi letu. Ni siku ambayo tunashuhudia mabadiliko ya muundo wa kiutawala na kiutendaji wa Jeshi letu ukizinduliwa rasmi kwa uzinduzi wa Kamandi ya Jeshi la Nchi Kavu. Sasa majukumu na mamlaka ya kiutendaji ya Jeshi letu lote yamepangwa kwa Kamandi. Pamoja na Kamandi hii tunayo Kamandi ya Jeshi la Anga na Kamandi ya Jeshi la Majini.
Kama mtakavyokumbuka, mapema miaka ya 80 tulikuwa na Kamandi mbili tu, yaani ya Ulinzi wa Anga na ya Wanamaji. Shughuli nyingine zote za Jeshi ambazo sasa tumezindua Kamandi yake ya Nchi Kavu, yaani Vikosi, Brigedi na wakati ule Divisheni za askari wa miguu zilikuwa zinafanywa Makao Makuu ya Jeshi. Kamandi mpya ya Jeshi la Nchi Kavu sasa ndiyo yenye jukumu la uongozi na usimamizi wa shughuli za kiutawala na kiutendaji za siku kwa siku za vikosi na brigedi. Makao Makuu ya Jeshi sasa yanabakia na majukumu ya msingi yanayohusu Jeshi zima ya sera, mikakati, na uratibu. Makao Makuu ya Jeshi yanahusika pia na masuala ya uwezeshaji wa Kamandi zake tatu na maslahi ya Wanajeshi kwa ujumla ili waweze kutimiza ipasavyo wajibu wao.
Nakupongeza sana CDF kwa uamuzi wako wa busara wa kufanya mabadiliko katika muundo wa Jeshi letu. Ni mabadiliko yanayoenda na wakati. Ndiyo maana sikusita kiyaunga mkono na kuyakubali. Nafarijika sana ninapoona Jeshi letu likijitahidi kuendeleza msukumo wa historia yake ya kubadilika kuendana na mabadiliko ya nyakati. Hiyo ndiyo siri kubwa ya uimara na mafanikio ya Jeshi letu.
Tangu Jeshi letu lianziswe mwaka 1964, limeshafanya mabadiliko mengi, ya kimuundo na kiutendaji kama matakwa ya kimazingira, kiutendaji na kiteknolojia yalivyojitokeza. Uzinduzi wa Kamandi hii unadhihirisha dhamira ya Jeshi letu ya kwenda na wakati. Mimi naamini ni mabadiliko yenye maslahi kwa Jeshi letu. Yatakaleta ufanisi na kuliimarisha Jeshi letu kwa utendaji kivita na kiutawala. Nawashukuru sana viongozi wa Jeshi na Wizara. Naomba muendelee kuwa wabunifu ili muendelee kufanya mabadiliko stahiki zaidi kwa nia ya kupata ufanisi mkubwa zaidi. Nasema tena hongereni sana.
Mheshimiwa Waziri, CDF, Makamanda na Askari;
Kuundwa kwa Kamandi hii, kunaleta uwiano wa kiutendaji kati ya Kamandi hii na Kamandi nyingine za Jeshi la Anga na Jeshi la Majini, hivyo kuongeza ufanisi katika utendaji wa Jeshi letu. Muundo huu pia, utasaidia kuleta ulinganifu wa mifumo ya Jeshi letu na majeshi ya nchi nyingine jirani katika jumuiya ya Afrika Mashariki na SADC na hata mataifa mengine rafiki duniani ambayo tunashirikiana nayo kwa mambo mbalimbali kama vile mazoezi na operesheni za pamoja. Hii itawasaidia wanajeshi wetu kushiriki kwa ufanisi zaidi kwenye mashirikiano hayo.
Ndugu Makamanda na Askari;
Wakati tunazindua Kamandi hii na kupongezana napenda kuwaomba muendelee kuwa wabunifu, mfikirie na kufanya mabadiliko zaidi yanayostahili ili muendelee kujiimarisha na kwenda na wakati. Ni muhimu kwa ajili hiyo mkaangalia miundo ya utumishi wa Jeshi, ikama, mitaala ya ufundishaji, zana na vifaa mbalimbali vya kijeshi ili navyo viendane na wakati. Napenda kuwahakikisheni kuwa Serikali itaendelea kuwaunga mkono katika jitihada zenu kadiri uwezo wa bajeti yetu utakavyoruhusu. Kwa moyo huo huo wa kuendelea kuwaunga mkono ndiyo maana nimekubali kuongeza umri wa kustaafu wa wanajeshi nchini kuwa miaka 60 badala ya 57 ya sasa. Mabadiliko hayo yatakayoanza Julai Mosi mwaka huu tunayafanya ili yaendane na wakati. Siku hizi watu wanachelewa kuzeeka tofauti na ilivyokuwa zamani,
Mheshimiwa Waziri; Naibu Waziri;
CDF, Makanda na Askari;
Nitakuwa mwizi wa fadhila kama sitaitumia nafasi hii, kwa mara nyingine kuwapongeza Wanajeshi wetu wote kwa kazi nzuri mnayoifanya ya kulinda uhuru na mipaka ya nchi yetu. Septemba Mosi, mwaka huu JWTZ litatimiza miaka 45 tangu kuasisiwa kwake. Imekuwa ni miaka 45 ya utumishi uliotukuka na mafanikio makubwa. Jeshi letu limetekeleza majukumu yake kwa ushujaa, umahiri, utii na uaminifu wa hali ya juu. Jeshi letu limezingatia kwa dhati misingi ya uweledi na uzalendo. Matokeo yake ni usalama na utulivu endelevu wa nchi yetu na watu wake. Tumefanikiwa kulinda mipaka ya nchi yetu wakati wote hata pale palipotokea tishio la wazi la nchi kuvamiwa na sehemu kutekwa na majeshi ya fashisti Idd Amin wa Uganda mwaka 1978. Nakumbuka Operesheni CHAKAZA mwaka 1978 – 1979. Nawapongeza sana.
Ndugu Makamanda na Askari;
Leo tunapozindua Kamandi hii, ninayo imani kubwa kwamba Jeshi letu litaendelea kujengeka na kwamba tutegemee mafanikio makubwa zaidi siku za usoni. Jeshi letu linaimarika zaidi na hivyo litaweza kutimiza vizuri zaidi jukumu lake la msingi la kulinda mipaka ya nchi yetu. Uimara utokao ogopesha wajinga wa nje na ndani kutothubutu kuchezea uhuru na mipaka ya nchi yetu. Jeshi letu pia litaendelea kutimiza ipasavyo wajibu wake wa kimataifa. JWTZ nao uzoefu wa kutosha na uweledi mkubwa katika nyanja za kimataifa. Limeshashiriki kwa ufanisi mkubwa katika operesheni nyingi, ndani na nje ya nchi. JWTZ limefundisha wapigania uhuru wa nchi za Kusini mwa Afrika wakati wa vita vya ukombozi. Sasa linaendekea kutoa mafunzo kwa wanajeshi wa nchi rafiki. JWTZ limeshiriki katika harakati na vita vya ukombozi na kuhami nchi marafiki.
Nazikumbuka operesheni KUMEKUCHA dhidi ya Wareno 1960, TEGAMA – Msumbiji, dhidi ya majeshi ya Rhodesia na Afrika Kusini, (1975 – 1980); SAFISHA – Msumbiji, dhidi ya RENAMO (1986 – 1988); Operesheni dhidi ya Mamluki waliovamia kisiwa cha Shelisheli mwaka (1981 – 1982) na hivi karibuni operesehni DEMOKRASIA huko Comoro mwezi Machi hadi Aprili, 2008 ya kumuondoa Kanali muasi Mohamed Bakar kutoka kisiwa cha Anjuan. Jeshi letu pia limekuwa linashiriki katika operesheni za kulinda amani chini ya Majeshi ya Umoja wa Mataifa. Hivi sasa tunajiandaa kwenda Darfur kwa ajili hiyo. JWTZ lina hazina kubwa ya uzoefu kutokana na operesheni hizo.
Ndugu Makamamanda na Wapiganaji;
Naomba nimalize kwa kuwashukuru tena, kwa kazi nzuri mnayoendelea kuifanya ya kulinda nchi yetu. Napenda kuwahakikishia kwamba Serikali inawajali na inathamini kazi yenu. Nawaomba msisahau kuwa siri kubwa ya mafaniko yetu Jeshini ni: Umoja, Ujasiri, Nidhamu na Uweledi. Yazingatieni. Nawatakia kila kheri katika majukumu yenu.
Asanteni sana.

No comments:

Post a Comment