HOTUBA YA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, MHESHIMIWA JAKAYA MRISHO KIKWETE, WAKATI AKIWAHUTUBIA WANANCHI WA DODOMA, NA WABUNGE KWENYE UKUMBI WA KILIMANI, DODOMA TAREHE 10 JUNI, 2009
Waheshimiwa Wabunge;
Ndugu wananchi;
Nawashukuru kwa dhati wazee wangu, Waheshimiwa Wabunge na wananchi wenzangu wa Dodoma, kwa kuitikia wito wangu wa kuja kukutana na kuzungumza nanyi. Nakushukuru Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa na Katibu wa Baraza la Wazee kwa maandalizi mazuri.
Mara kadhaa katika hotuba zangu za siku za nyuma, nimekuwa nikielezea jinsi ambavyo uchumi wa dunia unavyopita katika misukosuko mikubwa na jinsi ambavyo mtikisiko huo unavyoweza kuathiri uchumi wetu pia. Tayari athari zake tumezipata na tunaendelea kuathirika nazo. Nilifanya uamuzi siku za nyuma wa kuunda kikundi kazi cha watalaam chini ya uongozi wa Gavana wa Benki Kuu, Profesa Benno Ndulu, kufanya uchambuzi wa hali ilivyo ili kubaini athari tulizopata na kushauri hatua za kunusuru uchumi wetu na kujenga uwezo wa kujihami na kukuza uchumi.
Ndugu Wananchi;
Wenzetu hao wamemaliza kazi yao na taarifa yao imeshajadiliwa na Baraza la Mawaziri na maamuzi kufanywa. Matokeo yake ni kuwepo kwa mkakati wa Kunusuru Uchumi wa Tanzania dhidi ya Msukosuko wa Uchumi wa Duniani. Katika mkakati huo mpango wa utekelezaji wa malengo na hatua mbalimbali za kuchukua zimeanishwa.
Mtikisiko Katika Mfumo wa Fedha Duniani
Ndugu Wananchi;
Uchumi wa dunia unakabiliwa na matatizo makubwa sana ambayo hayajawahi kutokea kwa zaidi ya miaka 60. Mara ya mwisho uchumi wa dunia ulikuwa na matatizo makubwa katika miaka 1930 lakini nayo hayakuwa makubwa kama ilivyo safari hii. Matatizo ya uchumi wa dunia yana sura mbili. Upande mmoja lipo tatizo la kuvurugika kwa masoko na mfumo wa fedha wa kimataifa. Na, upande wa pili kudorora kwa uchumi wa dunia kulikosababishwa na kuanguka kwa masoko ya fedha na mitaji.
Tatizo hili limeanzia Marekani kutokana na udhaifu katika usimamizi wa mfumo wa fedha na hasa mikopo. Baadae ukaenea Ulaya Magharibi na hatimaye dunia nzima na siye tukiwemo. Kiwango cha athari kinatofautiana kutoka nchi moja na nyingine. Mataifa makubwa kiuchumi ya Marekani, Ulaya na Asia yameathirika zaidi kuliko nchi maskini za Afrika. Hata hivyo, mataifa makubwa yana uwezo mkubwa zaidi wa kukabiliana na athari hizo pamoja na ukubwa wake. Mataifa maskini kama yetu hayana uwezo wa kukabiliana hata na hizi athari ndogo zinazotukabili. Kinachoonekana kidogo kwao, kwetu sisi ni kikubwa.
Mabenki mengi, makubwa kwa madogo, na asasi za fedha kubwa na ndogo katika mataifa tajiri zimeshashuhudiwa zikianguka kibiashara au kufilisika. Masoko ya hisa na mitaji nayo hivyo hivyo yameanguka kwa kiasi ambacho hakijawahi kufikiwa. Makampuni mengi madogo na makubwa yameanguka. Watu wengi wenye hisa wamejikuta wakiharibikiwa na hata kuwa maskini bila kutazamia.
Makampuni mengi yameanguka kibiashara na kufilisika. Watu wamepoteza ajira kwa mamilioni na wengi wamepoteza nyumba na mali walizozipata kwa mikopo kwa sababu ya kushindwa kulipa mikopo. Kwa ujumla hali ya kiuchumi na kimaisha katika nchi hizo ni ngumu kwa makampuni mengi na watu wengi.
Kutokana na hali hii, uwekezaji umepungua, biashara ya ndani na nje imeshuka, uzalishaji viwandani umepungua sana na kwingine umesimama, makampuni madogo na hata makubwa na yenye heshima yamefilisika, ununuzi wa bidhaa umepungua, watu kwa mamilioni wakakosa ajira katika nchi kubwa kiuchumi. Athari hizo bado zinaendelea na matokeo yake ni kuzorota kwa ukuaji wa uchumi wa mataifa hayo makubwa na uchumi wa dunia kwa ujumla. Mwaka 2008, uchumi wa nchi hizi ulikua kwa asilimia 0.9. na mwaka huu inatarajiwa utapungua kwa asilimia 3.8.
Hali hii imezilazimisha Serikali za nchi hizo kuingilia kati na kutumia fedha za Serikali kuokoa makampuni binafsi, kinyume kabisa na falsafa ya soko huria. Vilevile, Serikali za nchi hizo zikalazimika kukopa fedha nyingi kwa ajili ya miradi mingi mikubwa ili kuchochea shughuli za kiuchumi.
Athari kwa Tanzania
Ndugu Wananchi,
Kwa upande wetu hapa nchini mabenki yetu yako salama kwa vile hatujafungamanishwa na masoko ya fedha ya kimataifa. Lakini, kibiashara na baadhi ya shughuli za kiuchumi, tumeathirika hasa zile zinazotegemea masoko ya kimataifa hususan ya mataifa tajiri ya Marekani, Ulaya na Asia. Athari kubwa ya kwanza ni ile ya kupungua kwa bei na masoko ya bidhaa zetu tunazouza nje ya nchi hususan mazao ya kilimo, madini na bidhaa za viwandani. Kadhalika, sekta ya utalii nayo imeathirika na kupungua kwa watalii wanaokuja nchini. Vilevile uwekezaji wa kutoka nje umepungua.
Kwa upande wa mauzo ya mazao ya kilimo napenda nitoe mifano ya pamba, kahawa na hata maua na karafuu. Kwa pamba, kwa kipindi kifupi cha miezi minne kuanzia Septemba 2008 bei ya pamba ilianguka kutoka senti 82 za dola kwa paundi moja mpaka senti 40. Hivyo pamba iliyonunuliwa kwa bei ya juu toka kwa wakulima, ghafla ilibidi iuzwe kwa bei ya chini na nyingine kukosa soko kabisa. Hadi mwezi Aprili 2009 marobota 124,344 ya pamba yalikuwa bado hayajauzwa. Inakadiriwa kuwa hasara iliyopatikana kwa kuuza pamba nje kwa bei chini ya bei ya kununulia ni kadiri ya shilingi bilioni 15 na 18. Unapochanganya tatizo hili na lile la pamba kutokuuzwa, shilingi bilioni 93.6 zilizokopeshwa na CRDB peke yake (bila kujumuisha riba) hazijarejeshwa. Kati ya madeni hayo, shilingi bilioni 4.6 ni ya vyama vya ushirika na TSh bilioni 81.9 ni ya makampuni 24 makubwa yanayofanya biashara ya pamba.
Vilevile, kwa upande wa zao la kahawa, kutoka mwezi Oktoba, 2008 bei zilianza kushuka kutoka wastani wa US$ 140 kwa gunia la Arabica hadi wastani wa US$ 104.21. Robusta nayo ilishuka toka wastani wa US$ 91 kwa gunia hadi dola za Marekani 64 ilipofika mwezi Machi 2009, ikiwa ni anguko la bei la asilimia 26 kwa Arabica na asilimia 29 kwa Robusta. Kahawa iliyokumbwa na msukosuko huo ni kiasi cha kilo 26,645,439 za Arabica zenye thamani ya US$ 55,536,099 na kilo 11,981,710 za Robusta zenye thamani ya US$ 15,469,353.
Kutokana na bei za kununulia kahawa hizo kwa mkulima (farm gate price) kuwa za juu kuliko ile ya kuuzia kwenye soko la dunia, vyama vya ushirika vya kahawa na wafanyabiashara walionunua kahawa wamepata hasara inayokadiriwa kuwa TSh bilioni 4.85.
Ndugu Wananchi;
Hasara waipatayo wanunuzi na ugumu waupatao kuuza mazao yao kunasababisha washindwe kulipa madeni yao Benki na kuwaweka kwenye hatari ya kufilisiwa mali zao walizoweka dhamana. Aidha, kwa ukubwa wa mikopo ambayo haijalipwa na ambayo huenda isilipwe itayafanya mabenki yaliyokopesha kupata hasara. Pia mabenki hayo yanaweza kukataa kuwakopesha wanunuzi wa mazao na kusababisha mgogoro mwingine mkubwa wa mazao ya wakulima kutokununuliwa msimu ujao. Jambo hilo likitokea litafanya wakulima kula hasara na kuwa maskini zaidi.
Shabaha ya mkakati wetu ni kumpunguzia mnunuzi mzigo wa hasara na madeni, kuiepusha benki na hasara na kuwezesha mazao ya mkulima kuendelea kununuliwa.
Kwa upande wa kilimo cha maua na mboga mambo ni hayo hayo. Bei imeshuka kwa asilimia 25 na mauzo yamepungua kwa sababu mahitaji katika masoko ya nje yamepungua kutokana na hali mbaya ya uchumi katika nchi hizo. Kuna hatari kwamba wakulima wa maua watashindwa kulipa mikopo ya mabenki ya Tshs. bilioni 43.4, ajira za watu zitapotea (tayari Mount Meru Flowers imepunguza watumishi 36). Sekta hii inaajiri watu 3,000 na wengi wao ni wanawake. Ni dhamira yetu pia hapa kuwanusuru wakulima, mabenki na ajira.
Madini
Ndugu Wananchi;
Hali ni mbaya pia kwa upande wa bei na masoko ya vito hasa almasi na Tanzanite. Bei ya Tanzanite imeshuka kwa asilimia hamsini na kufikia US$200 kwa karati. Bei ya almasi imeshuka kwa asilimia 26 na kuwa US$8,870 mwezi Septemba. Wachimbaji na wanunuzi wa almasi, Tanzanite na vito vinginevyo wanakabiliwa na tatizo kubwa la madini ambayo wanapata taabu kuyauza.
Bahati nzuri dhahabu haina matatizo hayo. Soko lake ni zuri na bei ni nzuri sana. Mkakati wetu unalenga namna ya kuwasaidia wachimbaji wa vito ambao tusipowasaidia wao na serikali tutaendelea kukosa mapato na wakati huo watu wengine watakosa ajira kwa sababu ya shughuli za uchimbaji kupungua.
Viwanda na Utalii
Ndugu Wananchi;
Viwanda vyetu navyo hasa vya nguo, nyuzi, mavazi na vile vya ngozi vimeathirika na msukosuko wa uchumi wa dunia. Mauzo nje yamepungua sana na kusababisha hasara kubwa. Uzalishaji umepungua, ajira nazo hali kadhalika.
Sekta ya Utalii ambayo ndiyo sekta kiongozi kwa mapato ya fedha za kigeni nayo imebanwa pia. Idadi ya Watalii wanaokuja nchini inapungua. Takwimu zinaonyesha idadi hiyo kupungua kwa asilimia 10. Mapato yatokanayo na utalii ya mwezi Januari – Aprili, 2009 nayo yamepungua na kufikia US$302.1 kutoka US$388.2 milioni mwaka 2008. Hali hiyo inaathari kubwa kwa wawekezaji na kwa mapato ya Serikali na fedha za kigeni hivyo nayo tumeipa uzito stahiki katika mkakati wa kunusuru uchumi.
Mapato ya Ndani
Ndugu wananchi,
Kutokana na matatizo ya kupungua mauzo nje, utalii, uwekezaji n.k mapato ya ndani ya Serikali nayo yameathirika. Sasa hivi, tunakusanya mapato kutoka ushuru wa forodha, kodi za ndani n.k yako chini ya kiwango tulichotarajia. Kama mwenendo wa makusanyo ya kodi utaendelea kama ulivyo sasa, makusanyo ya kodi kwa mwaka 2008/09 yatakuwa chini ya makadirio ya bajeti kwa asilimia 10. Kwa maneno mengine, tutashindwa kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 472.9 ambazo matumizi yake tulishayapangia kwenye bajeti. Katika mkakati huo tumeweka mipango ya kuikabili hali hiyo katika mwaka huu wa fedha na mwaka ujao pia ambapo tunadhani athari zitakuwepo au hata kuzidi.
Mapato ya Fedha za Kigeni
Ndugu Wananchi;
Kwa sababu ya kupungua kwa mauzo ya mazao yetu nje, mapato yetu ya fedha za kigeni yatapungua pia. Inakadiriwa kuwa thamani ya mauzo nje itapungua kutoka US$ 2,891 milioni mwaka 2008/09 hadi US$2,860 milioni mwaka 2009/10. Wakati huo huo mapato ya fedha za kigeni kutokana na utalii yatapungua kwa US$ 186 milioni. Katika mkakati wetu tunayo mipango ya kuziba pengo hilo ili kuepuka matatizo ya upatikanaji wa fedha za kigeni kwa ajili ya manunuzi yetu ya nje.
Uwekezaji kutoka nje
Ndugu Wananchi;
Kwa sababu ya matatizo ya uchumi uwekezaji wa vitega uchumi kutoka nje umepungua. Wawekezaji wamekuwa wanakosa fedha kutoka mabenki na masoko ya mitaji. Matokeo yake ni kuchelewa au kukosa kabisa au kuahirishwa miradi mikubwa ambayo ingetoa mchango muhimu kwa ukuaji wa uchumi wetu na ajira. Kwa mfano: Mradi wa umeme wa MW 300 kule Mtwara kwa sababu ya Barrick Gold Ltd. kujitoa na Artumas peke yake haina uwezo wa kifedha; mradi wa nickel Kabanga, mradi wa aluminium smelter, Mtwara; mradi wa usambazaji umeme mkoani Mtwara, miradi ya viwanda vya saruji na mbolea Mtwara na uwekezaji katika utafutaji wa madini umepungua kutoka US$90 mpaka US$40 milioni.
Ajira
Ndugu Wananchi;
Hali ya ajira nchini nayo itakuwa mbaya kutokana na matatizo haya. Mwaka 2009 ni mwaka ambao athari za msukosuko zimeanza kujitokeza kwa nguvu katika masoko ya ajira na kusababisha watu wengi kupoteza kazi na hivyo kuongeza umaskini wa kipato.
Hadi kufikia Aprili 2009 jumla ya wafanyakazi 48,000 walikuwa wamepoteza ajira zao nchini. Kutokana na kutarajiwa kupungua kwa idadi ya watalii wanaokuja nchini, baadhi ya hoteli zilizotarajiwa kuwapokea watalii hao zimelazimika kupunguza wafanyakazi wao kutokana na kupungua kwa biashara. Kati ya asilimia 20-30 za ajira katika sekta ya utalii ZanzĂbar ziko hatarini kupotea kutokana na upungufu wa utalii.
Vivyo hivyo, katika sekta ya kilimo, viwanda na madini, watu wengine wanatarajiwa kupoteza kazi zao.
Kupungua kwa ukuaji wa uchumi
Waheshimiwa Wabunge, Ndugu Wananchi,
Matokeo ya athari zote hizi ni kupungua kwa kasi ya ukuaji wa uchumi nchini. Kama mjuavyo, katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, uchumi wetu umekuwa ukikua kwa kiwango cha juu cha wastani wa asilimia 7.2. Tulitegemea mwaka huu uchumi wetu ungekuwa kwa zaidi ya asilimia 8 na kufikia asilimia 10 mwaka 2010 kama tulivyoahidi kwenye Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2005. Lakini kama wasemavyo Waswahili, ng’ombe wa maskini hazai. Msukosuko wa fedha na uchumi duniani umesababisha ukuaji wa uchumi wa Tanzania kupungua kutoka asilimia 7.4 mwaka jana hadi kati ya asilimia 5-6 mwaka huu. Kwa upande wa Zanzibar, uchumi wao unategemewa kukua kwa asilimia 4.5 mwaka huu ukilinganisha na asilimia 5.4 mwaka jana.
Mkakati wa Kuhami na Kuunusuru Uchumi
Ndugu Wananchi;
Baada ya kutafakari hali hii, na kuchambua athari hizi nilizobainisha kwa uchumi, ustawi na mipango ya muda mrefu ya maendeleo ya Taifa letu, na kwa kuzingatia azma yangu niliyoitangaza kwenye salamu ya mwaka mpya wa 2009, kwamba mwaka huu ni mwaka wa kuhami na kukuza uchumi, tumebuni na tutatekeleza Mkakati Maalum wa Kuhami na Kuunusuru Uchumi wa Tanzania.
Mkakati huu unazingatia ukweli kuwa msukosuko wa uchumi duniani ni wa kupita. Changamoto ya muda mfupi ni jinsi ya kujinusuru na hatimaye kudumisha juhudi za maendeleo baada ya msukosuko kupita.
Katika kukabili athari hizi nilizozitaja, tunalenga mambo mawili makuu. Kwanza ni kupunguza makali ya msukosuko, na pili, kulinda uwekezaji ambao ni muhimu katika kudumisha ukuaji endelevu wa uchumi katika kipindi cha muda wa kati.
Mkakati wetu wa kuhami na kuunusuru uchumi unalenga kukabili matatizo ya mpito na dharura – hasa ya ukwasi (liquidity) na siyo ufilisi (solvency). Mkakati huu sio mbadala wa mipango ya maendeleo na bajeti ya Serikali ya kila mwaka. Chini ya mkakati huu Serikali imepima matatizo kwa uzito wake na kushughulikia yale tu yaliyojitokeza hivi karibuni kutokana na msukosuko wa uchumi na siyo vinginevyo.
Ndugu Wananchi;
Tumetengeneza Mkakati huu kutimiza malengo makubwa manne:
1. Kulinda ajira na vipato vya wananchi;
2. Kuhakikisha upatikanaji wa chakula;
3. Kulinda uwekezaji muhimu katika miradi ya maendeleo, hususan miundombinu, na
4. Kulinda programu muhimu za kijamii
Ndugu Wananchi;
Kama nilivyosema, lengo kuu la kwanza la mkakati huu ni kupunguza makali au kuhimili shinikizo la msukosuko, hususan kuwalinda wananchi walio katika hatari kubwa zaidi ya kimaisha. Katika kutekeleza hili lengo yako mambo kadhaa ambayo tutayafanya:
(i) Kufidia hasara waliyopata wanunuzi wa mazao msimu wa 2008/09
Serikali imeamua kufidia vyama vya ushirika na makampuni yaliyonunua mazao ya wakulima na kuyauza kwa hasara. Hasara hiyo inayokisiwa kufikia shilingi 21.9 bilioni imepatikana kutokana na bei ya kuuzia mazao hayo kuwa chini sana ya gharama iliyotumika kuyanunua. Serikali italipa madeni yenye thamani ya hasara hiyo, moja kwa moja kwa mabenki yaliyokopesha vyama na makampuni hayo. Lakini tutafanya uhakiki kabla ya kulipa. Napenda kusisitiza kuwa hatutalipa madeni ya zamani ambayo hayahusiki na msukosuko wa uchumi wa dunia.
(ii) Kutoa udhamini wa kuahirisha mikopo ya waathirika
Yapo madeni ambayo wakopaji kwa sababu ya msukosuko wa uchumi wa dunia wanapata matatizo kulipa kwa wakati. Kundi hili linawajumuisha wengi wenye viwanda, wenye shughuli za utalii, kilimo n.k. Madeni hayo yanafikia Shs.270 bilioni.
Serikali itayadhamini madeni na kuyataka mabenki kuahirisha ulipaji wa mikopo hiyo na riba yake wa miaka miwili. Udhamini wa Serikali utatolewa kwa uwiano wa kila shilingi moja kwa shilingi tano na Serikali ikidhamini asilimia 70 ya mkopo. Kwa uwiano huu, fedha zitakazohitajika katika dhamana hiyo ni TSh 45 bilioni. Pamoja na kutoa nafuu kwa makampuni lakini hatua hii pia itayawezesha mabenki kuendelea kutoa mikopo na hivyo shughuli za kiuchumi na biashara hazitaisimama.
(iii) Kutoa mitaji ya uendeshaji (working capital) kwa riba nafuu
Tumeamua vilevile kuchukua hatua za kupunguza upungufu wa mitaji ya uendeshaji (working capital). Kwa ajili hiyo Serikali itayakopesha mabenki fedha kwa riba nafuu ya asilimia 2 ili na wao wawakopeshe wafanyabiashara fedha za mitaji ya uendeshaji kwa riba nafuu. Lengo ni kusaidia walioko kwenye sekta zinazokumbwa na msukosuko wa uchumi waweze kuhimili vishindo. Kwa kila shilingi moja tutakayotoa sisi Serikali, benki husika itatakiwa itoe shilingi moja na nusu (1:1½).
Kwa madhumuni haya, tutaanzisha mfuko maalumu wenye shilingi bilioni 80 ambao utasimamiwa na Benki Kuu na mabenki yatakayoshiriki yatatakiwa kutoa shilingi 120 bilioni. Viwango vya riba kwa wakopaji vitapangwa kwa maelewano ya pamoja baina ya BoT na mabenki na itategemea sekta na shughuli yenyewe.
(iv) Kuboresha Mifuko ya Dhamana:
Chini ya mkakati huu tutaiboresha na kuiongezea fedha mifuko ya kudhamini mikopo (credit guarantee schemes). Mifuko hiyo ni pamoja na Mfuko wa Udhamini wa Uuzaji wa Mazao Nje ya Nchi (Export Credit Guarantee Scheme -ECGS) na Mfuko wa Udhamini wa Mikopo kwa Wajasiliamali Wadogo na wa Kati (SME Credit Guarantee Scheme). Tutaongeza mtaji wa shilingi bilioni 10 kwa kila mfuko katika mwaka wa fedha wa 2009/10. Nyongeza hii itawezesha kuongeza dhamana ya mikopo ya shilingi bilioni 65 kwenye Mfuko wa Udhamini wa Uuzaji wa Mazao Nje ya Nchi na shilingi bilioni 60 kwenye Mfuko wa Udhamini wa Mikopo kwa Wajasiliamali Wadogo na wa Kati katika kuchochea mauzo ya bidhaa nje na uzalishaji. Hivi sasa mfuko wa ECGS una mtaji wa Shs.32.5 bilioni na umekopesha Shs.161.5 bilioni na ule wa SME una Shs.500 milioni na umeshakopesha Shs.6.5 bilioni.
(v) Kupunguza gharama za vito vya thamani:
Katika sekta ya vito vilivyoshuka bei kwa kiasi kikubwa, kama vile Tanzanite na almasi, tunaangalia uwezekano wa kuahirisha ulipaji wa mrahaba (royalty) kwa wachimbaji wa vito. Lengo ni kuwapa muda wa kupumua na kujijenga. Chini ya mpango huu Serikali itaahirisha mapato ya kiasi cha US$ milioni 0.5 kutoka almasi na US$ milioni 2.5 kutoka tanzanite.
(vi) Kuongeza uzalishaji wa Chakula
Ndugu Wananchi;
Lengo lingine muhimu la mkakati huu ni kuinusuru nchi kutokana na athari za upungufu wa chakula duniani zilizochochewa na msukosuko. Katika kutekeleza hili, mkakati huu utahakikisha kuwa miradi yote ya kilimo, hususan ile ya uzalishaji wa mazao ya chakula, inaendelea kugharimiwa bila kuathiriwa na msukosuko. Lengo la kwanza ni kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula ili kujitosheleza kwa chakula na kuuza ziada nje na hivyo kutumia ipasavyo fursa inayotokana na kuadimika kwa chakula duniani.
Chini ya mkakati huu, pamoja na kuendelea kuhimiza na kusimamia yale mambo yote ya kuongeza tija na uzalishaji kwenye kilimo, tumeamua katika kipindi hiki kufanya yafuatayo: (i) kutoa mikopo nafuu na ya muda mrefu ya shilingi 20 bilioni kupitia TIB kwa sekta binafsi kwa ajili ya kuendeleza kilimo (ii) kutoa shilingi bilioni 20 kwa ajili ya mkopo wa riba nafuu kwa zana za kilimo kama matrekta madogo kupitia mpango wa karadha (lease finance), ambapo, kwa kila shilingi ambayo serikali itatoa, mabenki yatakayoshiriki katika mkakati huu itabidi nayo yatoe shilingi moja: na (iii) Kuongeza kiasi na idadi ya wakulima watakaopata mbolea ya ruzuku kwa utaratibu wa vocha. Benki ya Dunia watatupa mkopo wa US$46 milioni na sisi tutatoa kiasi hicho hicho kwenye mfuko wa mbolea katika mwaka ujao wa fedha (2009/10).
Aidha tumeamua sasa tutumie Hifadhi ya Chakula ya Taifa kusaidia kutuliza bei za vyakula kwa walaji. Tunaiboresha sera ya sasa ambapo Hifadhi hungojea ilani ya njaa. Tumesema kupanda sana kwa bei za vyakula vikuu katika soko ni dalili ya upungufu hivyo kupunguza makali kila inapowezekana. Chini ya mkakati huu, tutatoa shilingi bilioni 20 kwa Hifadhi ya Chakula ya Taifa kwa ajili ya kuongeza akiba ya chakula na kudhibiti mfumuko wa bei.
Miundombinu
Ndugu Wananchi,
Kuhusu lengo la kulinda uwekezaji muhimu, hasa katika miundombinu, ya umeme na reli tumekubaliana kuwa tuendeleze juhudi za kutafuta mikopo kutoka Benki ya Dunia na mashirika mengine ya fedha. Kwa ajili hiyo tutatumia fedha za IMF kukwamua mradi wa usambazaji umeme Mtwara. Zinatakiwa US$ 7 milioni. Kuhusu Shirika la Reli, sisi tuchangie sehemu yetu, yaani US$43 milioni, kuongezea US$ 40milioni za Benki ya Dunia kuimarisha reli yetu. Wakati huo suala la uendeshaji tulitafutie jawabu muafaka.
Kadhalika tumekubaliana kuwa taendelee kuwekeza katika ujenzi wa barabara na miradi ya elimu, afya na maji. Suala la hati-fungani ambalo liliahirishwa kwa sababu ya matatizo ya soko la fedha tulitafutie vyanzo mbadala.
Ndugu Wananchi;
Tumekubaliana pia katika mkakati huu, kuwa lazima kuhakikisha kuwa utulivu wa uchumi unakuwepo ili kuhimiza ukuaji endelevu wa uchumi na kuvutia sekta binafsi kushiriki. Vilevile tuongeze kasi ya kuharakisha uimarishaji wa TIB na uanzishwaji wa Agricultural Development Bank.
Ndugu Wananchi;
Kuhusu lengo la Mkakati la kulinda programu muhimu za kijamii, Serikali itahakikisha kuwa mipango yote ya kijamii haitaathirika, hata ile ambayo itakosa fedha za kutosha kutoka kwa wafadhili. Hii inajumuisha mipango ya utoaji wa ruzuku kwa dawa za kurefusha maisha kwa wagonjwa wa UKIMWI, vyandarua vya kuzuia malaria, programu za kifua kikuu, na nyingine za kusaidia juhudi za vijana na kulinda makundi ya wanyonge.
Ndugu Wananchi;
Pia zipo hatua kadhaa nyingine za kisera ambazo Serikali inaziandaa katika kukabiliana na athari za msukosuko huu. Katika miezi inayokuja, Wizara mbalimbali zitatangaza hatua za kisera zenye nia ya kuzihami sekta hizo na athari hizi na kuchochea ukuaji wa sekta mbalimbali kama vile utalii na viwanda. Miongoni mwa hatua tunazoziandaa sasa ni kupunguza gharama za visa kwa watalii kutoka dola 100 na 200 na kuwa dola 50. hazina inaangalia uwezekano wa kufanya hivyo.
Namna Serikali Itakavyolipia Gharama za Programu Hii
Ndugu Wananchi;
Kutekeleza Mkakati huu ni gharama kubwa. Zitahitajika kiasi cha shilingi bilioni 1,692.5. Tumetenga pesa hizo katika Bajeti yetu ya mwaka wa fedha utakaoanza Julai, 1, 2009. Sehemu kubwa ni fedha zetu lakini pia tutapata misaada kutoka kwa marafiki zetu wa maendeleo hasa Benki ya Dunia, IMF, EU na India.
Hitimisho
Ndugu Wananchi,
Sasa nimefika mwisho wa hotuba yangu. Nawashukuru tena kwa kukubali wito wangu. Kwa nchi yetu ambayo bado ina safari ndefu katika maendeleo, hatua tuliyochukua hapa ni kubwa na ya kihistoria. Katika kuchukua hatua hii, tumezingatia mahitaji ya dhamana tuliyopewa na wananchi katika kuwaongoza na kusimamia maendeleo na ustawi wao na wa nchi yetu. Lakini vilevile, tumezingatia mafundisho ambayo historia ya nchi yetu imetupatia. Kwa mkakati huu, tumedhamiria kuepuka hali iliyojitokeza miaka ya 1980 ambapo kutokana na kushindwa kukabili kwa dhati na wakati muafaka, athari za kupanda kwa bei za mafuta na hali mbaya ya uchumi wa dunia iliyofuatia, zilisababisha nchi kupoteza miongo miwili ya ukuaji wa uchumi na mafanikio yaliyokuwa yamepatikana katika nyanja za jamii na miundombinu.
Mwisho kabisa, nawasihi viongozi wenzangu na wananchi kwa ujumla, tuwe wavumilivu na tuiunge mkono Serikali katika kutekeleza mkakati huu. Tangu mwaka 2006, mambo hayakuwa mepesi sana, tumepitia misukosuko mikubwa kwa uchumi wetu: mgao mkubwa wa umeme, njaa, bei kubwa ya mafuta na bei kubwa za vyakula na sasa msukosuko huu wa aina yake. Kwa kila tatizo tumepambana nalo kiume na kwa umakini mkubwa na kuvuka salama. Mshikamano wetu, umoja wetu ndiyo uliotufikisha hapo.
Napenda kuwahakikishia wananchi wa Tanzania kwamba Serikali yao inawajali na inafanya kila lililo ndani ya uwezo wake kutimiza wajibu wake katika kuwatumikia.
Sisi katika Serikali tupo kwa ajili yenu na tutaendelea kuwatumikia kwa nguvu zetu zote. Tutaendelea kutengeneza mipango na mikakati ya kukabiliana na matatizo na changamoto zinazowakabili wananchi wa Tanzania walioko katika kila kona ya nchi yetu. Tuliyaweza yale naamini na haya tutayamudu!!
Asanteni sana kwa kunisikiliza!
Mungu Ibariki Afrika!
Mungu Ibariki Tanzania!
Friday, 12 June 2009
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment