HOTUBA YA MHE. JAKAYA MRISHO KIKWETE, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, KWENYE UZINDUZI WA KIVUKO CHA MV. MAGOGONI 4 JUNI 2009
Mheshimiwa Dk. Shukuru Kawambwa (Mb), Waziri wa Miundombinu,
Waheshimiwa Mawaziri,
Ndugu Viongozi na Watendaji wa Serikali,
Viongozi wa vyama vya siasa,
Ndugu Wananchi wenzangu,
Wageni waalikwa,
Mabibi na Mabwana,
Awali ya yote, napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa kunialika kuja kujumuika nanyi hapa katika uzinduzi wa kivuko kipya cha Mv. Magogoni.
Nawapongeza sana wananchi wa Kigamboni na wa jiji la Dar es Salaam kwa jumla kwa kupata kivuko kipya kiitwacho MV. Magogoni. Kivuko hichi kipya, kikubwa na cha kisasa tumekinunua kutoka Ujerumani kwa gharama ya shilingi 8.5. bilioni. Kimetatua tatizo kubwa lililokuwa linawasumbua watu waliokuwa wanavuka kutoka au kwenda Kigamboni.
Kwa muda mrefu, wananchi wa Kigamboni wamekuwa wakipata adha ya usafiri, maisha yao kuwa hatarini na usalama wa mali zao kuwa mashakani. Vivuko vilivyokuwepo MV. Alina na MV. Kigamboni vilikuwa vimechakaa sana hivyo kushindwa kufanya kazi ipasavyo. Kwa kweli vilikuwa tishio kwa kila hali. Wakati wa kampeni za uchaguzi wa mwaka 2005, Chama cha Mapinduzi kiliahidi kupitia Ilani yake kutatua tatizo la vivuko kadhaa nchini, kimojawapo kikiwa hiki cha Kigamboni. Leo hii tunasherehekea kutimia kwa ahadi yetu kwa wananchi wa Dar es Salaa hasa wale waishio na waendao Kigamboni.
Kadhalika tumeshatimiza ahadi kwa wananchi wa Mwanza kwa kivuko cha Busisi (MV. Misungwi), kivuko cha Kisiwa cha Kome (MV. Kome) na kivuko cha kati ya Bugorora na Ukara (MV. Nyerere). Kwa wananchi wa Ruvuma kuna kivuko cha MV. Ruhuhu na wa Morogoro kivuko cha mto Kilombero.
Kivuko hiki tunachokizindua rasmi leo ndicho kikubwa kuliko vivuko vyote nchini. Kina uwezo mkubwa wa kubeba tani 500 yaani Magari 60 na abiria 2000 kwa wakati mmoja. Kwa kuwa na kivuko hiki tatizo la usafiri sasa siyo gumzo tena. Ifikapo mwezi Septemba, 2009 tatizo litakuwa limekwisha kabisa pale kivuko cha MV. Kigamboni kitakapoanza kazi. Hivi sasa kivuko hicho kinafanyiwa matengenezo makubwa kukirudisha katika kiwango cha juu cha ubora. Kadhalika kule Bususi, Mwanza nako matengenezo ya kivuko cha MV. Sengerema yatakapokamilika shughuli ya uvushaji watu kati ya Kigongo na Busisi katika Ziwa Victoria itakuwa imeimarika sana.
Ndugu Wananchi,
Nimefurahi kusikia kuwa ujenzi wa Kivuko Mv. Magogoni umefanyikia hapa Dar es salaam eneo la Bandari na kuweza kuwapatia ajira vijana 30 ambao wamejifunza na kupata maarifa na ufundi mpya wa ujenzi wa vivuko na hata maboti. Ninaamini kwa uzoefu walioupata wataweza kujiajiri wenyewe kwa kujenga vivuko na boti ndogondogo za uvuvi ili kujipatia riziki na kuboresha hali ya maisha yao.
Serikali itaendelea na utaratibu huu wa kujenga vivuko hapa nchini ili kutoa huduma nzuri ya usafiri wa majini na kuendeleza teknolojia ya ufundi wa kutengeneza vivuko hapa nchini, na kukuza ajira kwa vijana wetu.
Ndugu wananchi,
Ziko sehemu nyingi za nchi yetu ambako kufikika kwake ni kwa vivuko tu. Serikali imedhamiria kuhakikisha kuwa vivuko vyote nchini vinakuwa vya uhakika na salama kwa matumizi ya wananchi kwa kuvikarabati na kununua vipya pale vinapohitajika kadri uwezo wa bajeti ya serikali unavyoruhusu.
Katika kutekeleza hayo, Serikali kwa sasa inakarabati vivuko viwili vya Mv. Kigamboni hapa Dar es Salaam, na Mv. Sengerema huko Mwanza. Aidha, tumenunua vivuko vipya sita vya Kilombero huko Morogoro, Kivuko cha Mv. Nyerere kinachohudumia kati ya Bugorora na Ukara Mkoani Mwanza, Mv. Ruhuhu Mkoani Ruvuma, Mv. Misungwi kinachohudumia kati ya Kigongo hadi Busisi huko Mwanza na Mv. Kome II kinachofanya kazi kati ya Kisiwa cha Kome kwenda Nyakalilo. Vilevile, tutanunua vivuko vipya vya Musoma kwenda Kinesi Mkoani Mara ambapo wananchi wa Kinesi watakwenda Musoma mjini kwa kutumia kivuko kwa muda wa dakika 30 badala ya kuzunguka Kilometa 54, pia tunanunua vivuko vingine vipya vya Rugezi hadi Kisorya Wilayani Ukerewe, Utete mkoani Pwani na Pangani mkoani Tanga.
Vilevile, katika mipango ya miaka mitatu ijayo, Serikali inatarajia kununua vivuko vifuatavyo kuanzia 2009/10:
1. Kivuko cha tani 50 katika maeneo ya Kilambo - Mtwara. Kivuko hiki kitarahisisha usafiri eneo la mwambao wa kati ya Mtwara Tanzania na Msumbiji
2. Kivuko cha tani 50 kitakachotumika kati ya Msanga Mkuu na Mtwara Mjini ambapo kitapunguza usumbufu wa wananchi kuzunguka Km 20 kufika Mtwara.
3. Kivuko cha Mto Rusumo – Ngara Kagera ambapo kitapunguza Km 60 za kuzunguka kuja Bukoba Mjini.
4. Kivuko cha Kyela – Itungi Port wananchi watatumia nusu saa kusafiri kwa kivuko badala ya kuzunguka kwa Km 70 kufika Kyela.
Ndugu wananchi,
Kuna sehemu ambazo tunatumia vivuko kwa sababu ya kujenga madaraja haiwezekani kwa jinsi maumbile yake yalivyo. Lakini zipo sehemu ambazo tunatumia vivuko lakini madaraja yanawezekana kujengwa. Tunachelewa kujenga madaraja kwa sababu ya gharama kubwa na uwezo wetu mdogo wa fedha. Tunayo dhamira ya kujenga madaraja kidogo kidogo katika sehemu hizi.
Moja ya madaraja ambayo tumeshafanya uamuzi wa dhati kabisa kujenga ni Daraja la Kigamboni. Mipango ya ujenzi wa daraja hili imekuwapo tangu uhuru. Lakini sasa tumedhamiria kufanya. Tumeahidi katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM Ibara ya 44 (f) kwamba, katika kipindi cha miaka mitano tuwe tumeanza maandalizi ya ujenzi wa daraja hili. Nafurahi kwamba tutatimiza ahadi hiyo. Na tutafanya hivyo kwa kushirikiana na wenzetu wa sekta binafsi.
Tuko kwenye hatua nzuri za maandalizi. Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF) lipo kwenye mchakato kumpata Mtaalam Mshauri ili atayarishe nyaraka za zabuni. Matumaini yetu ni kwamba, ifikapo mwezi Septemba mwaka huu, nyaraka hizo zitakuwa tayari. Mambo yote yakienda kama yalivyopangwa, basi ujenzi wa daraja unaweza kuanza katika mwaka wa fedha wa 2010/2011. Daraja hili litafungua kwa kiasi kikubwa fursa za uchumi na uwekezaji huko Kigamboni.
Vilevile, kwa sasa, tunafanya usanifu wa ujenzi wa daraja tuliloliahidi kwenye ibara ya 44 (i) ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM wa 2005, yaani Daraja la Mto Kilombero ili kuunganisha Wilaya za Kilombero na Ulanga.
Ndugu wananchi,
Hata hivyo, kujenga daraja kuvuka ng’ambo pekee hakutoshi kama barabara za Kigamboni haziko katika hali nzuri. Kwa kutambua hilo tunajenga barabara kwa kiwango cha lami kutoka Kivukoni hadi Mjimwema mpaka Kongowe. Barabara nyingine tutakayojenga kwa lami ni ya kutoka Kivukoni hadi Tungi na nyingine ni ile ya kutoka Mjimwema hadi Pembamnazi. Wakati tunajenga barabara hizi kwa lami, tutaendelea kuimarisha barabara nyingine za Kigamboni, kama ile ya Tungi hadi Kibada.
Ndugu wananchi,
Ukiacha hili la Kivuko ambalo tumelitimiza na barabara za Kigamboni, Serikali inaendelea na jitihada za kupunguza matatizo ya ya usafiri na usafirishaji katika Jiji la Dar es Salaam. Hivi sasa tunaelekeza nguvu zetu katika kujaribu kupunguza msongamano wa magari katika barabara za Dar es Salaam.
Kwa ajili hiyo, zipo barabara ambazo tunazifanyia ukarabati mkubwa ili zirudi katika hali yake ya zamani, kama tufanyavyo kwa barabara ya Mandela. Baadhi tunazijenga upya na kuzipanua kama ilivyo kwa barabara ya Sam Nujoma na barabara ya Kilwa. Nyote ni mashahidi wa kazi inayoendelea kufanyika katika barabara hizo.
Vilevile ziko barabara kadhaa za Dar es Salaam ambazo hivi sasa ni za udongo ambazo tumeamua tutazijenga kwa kiwango cha lami. Nia yetu kuu ni kupunguza msongamano katika baadhi ya mabarabara kwa kutoa fursa kwa magari kuchepukia barabara hizo. Tumekwishatoa kiasi cha shilingi bilioni 20 kwa ajili ya ujenzi na upanuzi wa barabara hizi. Baadhi ya barabara hizo ni pamoja na zifuatazo:
1. Barabara ya kutoka Ubungo Bus Terminal hadi Kigogo Roundabout, na kutoka Kigogo Roundabout hadi Mtaa wa Twiga Jangwani. Maombi yangu ni kwamba wasiue viwanja vya michezo vya Jangwani.
Nimeambiwa kuwa mikataba ya ujenzi wa barabara hizi itasainiwa wakati wowote wiki ijayo na ujenzi kuanza mara moja.
2. Barabara nyingine ni ile ya kutoka Tabata Dampo hadi Kigogo;
3. Vilevile iko barabara ya kutoka Ubungo Maziwa hadi Mabibo External;
4. Barabara ya kutoka Jet Club hadi Vituka hadi Davis Corner ya umbali wa kilomita 12;
5. Barabara ya kuanzia Mbezi Mwisho hadi Barabara ya Nyerere Ukonga Banana kupitia Malamba Mawili na Kinyerezi. Barabara hii itawezesha magari yanayotoka viwandani maeneo ya Nyerere Road kuweza kuanza safari za mikoani au nchi jirani bila kupitia Ubungo.
6. Barabara ya kutoka Tegeta Kibaoni hadi Mbezi Mwisho (Morogoro Road) kupitia Goba. Barabara hii itawawezesha wachukuzi wa saruji kutoka kiwandani Wazo Hill kwenda mikoani au nchi jirani bila kupitia mjini. Vilevile itawezesha wakazi wengi wa maeneo ya Bagamoyo Road, Tegeta na Mbweni kuweza kusafiri mikoani bila kupitia mjini.
7. Tunao mpango wa kutengeneza kwa lami barabara kutoka Tangi Bovu hadi Goba
8. Vilevile tunao mpango wa kupanua njia mbili kipande cha barabara kutoka njia panda ya Morocco hadi Kawe kuungana na barabara ya Bagamoyo kupitia Shoppers Plaza, kupitia Mikocheni na Mlalakua ili kupunguza msongamano mkubwa wa kipande kile cha barabara. Pia kuunganisha kipande cha kutoka Tume ya Sayansi hadi Msasani kwa Mwalimu Nyerere kwa barabara ya njia mbili.
9. Pia barabara ya Kimara Kinguruwe hadi Mabibo External nayo tutaijenga kwa lami. Barabara hii ya kilomita 9 itawezesha watu kupita kuja na kutoka mjini bila kupitia Ubungo;
10. Vilevile, ipo mipango ya kutengeneza kwa lami barabara ya Kimara Baruti hadi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kupitia Msewe na Changanyikeni.
11. Tumefanya mazungumzo mazuri na Serikali ya Japan wakati wowote tutapata majibu kuhusu utoaji fedha kwa ajili wa upanuzi wa barabara ya kutoka njia panda ya Morocco Road hadi Tegeta Kibaoni ambayo itapunguza sana msongamano wa magari Jijini.
Ndugu wananchi,
Nimeona niwape taarifa ya barabara hizi ili mjue hatua tunazochukua kupunguza tatizo la usafiri Dar es Salaam.
Usalama wa Vyombo vya Majini
Ndugu wananchi,
Hali ya usalama wa vyombo vya majini imekuwa siyo ya kuridhisha hata kidogo. Matukio ya ajali za vyombo vya majini hapa nchini yamekuwa mengi mno. Katika kipindi cha kuanzia Januari, 2006 hadi Desemba 2008 yamekuwepo matukio 28 ya ajali zilizo sababisha vifo vya watu 149 na 240 kuokolewa. Majuzi tena kumetokea ajali ya Meli ya Mv. Faith iliyopinduka katika Bandari ya Malindi kule Zanzibar.
Tathmini zinaonyesha kuwa ajali hizo zimekuwa zinasababishwa na ubovu wa vyombo unaochangiwa na umri mkubwa na matengenezo yasiyoridhisha, makosa ya kibinadamu na hali mbaya ya hewa. Wakati mwingine pia uelewa mdogo wa umuhimu na matumizi ya vifaa vya kuokolea umechangia vifo vya watu.
Serikali iliunda SUMATRA kwa nia ya kuboresha usimamizi wa uendeshaji wa vyombo vya majini ili kuongeza usalama wa usafiri majini. Tunaipongeza SUMATRA kwa kazi kubwa na nzuri ambayo imekuwa inafanywa tangu kuundwa kwake mpaka sasa. SUMATRA imeweka maafisa wasimamizi katika maeneo mbalimbali nchini ikiwa ni pamoja na Mwanza, Bukoba, Sumbawanga, Kigoma na Dar es Salaam. Hata hivyo, lazima SUMATRA waongeze udhibiti wa vyombo vinavyosafiri majini. Wawe makini zaidi katika kusimamia ubora wa vyombo hivyo, ujuzi wa manahodha na wafanyakazi wake, ubora wa huduma stahiki kwa abiria ikiwamo zile za kuokolea abiria panapotokea ajali.
Aidha SUMATRA iendelee kutoa mafunzo kwa wamiliki na waendesha vyombo vya usafiri majini ili kuwaongezea ufahamu juu ya umuhimu wa kuzingatia taratibu na kanuni zinazosimamia uendeshaji wa vyombo hivyo.
Ndugu wananchi,
Katika kuimarisha uwezo wetu wa kuzuia na kukabiliana na majanga kwenye maji, Serikali imejenga mnara wa kuongozea meli katika eneo la Magogoni ambao una kituo cha kuratibu shughuli za utafutaji na uokoaji pamoja na kuratibu matukio ya uharamia baharini. Kituo hiki kimezinduliwa mwezi Machi, 2009 na kwa muda mfupi wa uwepo wake, kimeweza kuratibu zoezi la utafutaji na uokoaji wa meli ya Comoro iliyopata ajali ikiwa safarini kutoka Dar es salaam kwenda Comoro tarehe 16 Aprili, 2009. Katika zoezi hilo watu 77 waliokolewa.
Ndugu wananchi,
Kabla sijamaliza, naomba niongelee uvumi ambao umeenea sana ndani ya jamii yetu, hasa kwa wakazi wa Kigamboni. Kumekuwa na upotoshaji mkubwa kwamba eneo zima la Kigamboni limeuzwa kwa wawekezaji. Wapo wanaodai kuwa Kigamboni imeuzwa kwa watu maarufu wa Marekani na wapo wanaodai kwamba imeuzwa kwa watu maarufu kutoka Uarabuni. Mwanzoni niliposikia maneno hayo niliyapuuza. Lakini nikagundua kuwa yameenea sana na yanaaminiwa na watu wengi hata wale ambao ungedhani wana uelewa wa juu wa mambo. Nikamuagiza Waziri wa Ardhi atoe ufafanuzi.
Ningependa nami kurudia kwamba hakuna ukweli kabisa katika uvumi huo. Ninachokijua mimi ni kuwa Jiji Dar es Salaam likishirikiana na Serikali Kuu (Wizara ya Adhi, Nyumba na Makazi) inao mpango kabambe wa kuufanya Kigamboni kuwa Mji Mpya. Hii ni kwa maana ya kwamba uwe umepangwa na kujengwa kisasa. Nia ni nzuri ya kuendeleza Kigamboni na jiji la Dar es Salaam kwa jumla hasa sasa ambapo kutajengwa daraja hivyo kushawishi watu wengi zaidi kupenda kuhamia na kuishi huko.
Tatizo kubwa la Dar es Salaam ni kuwa na nyumba nyingi kujengwa maeneo yasiyopimwa na kupangwa vizuri. Hali hii haikubaliki, tusiiache iendelee hivi. Na tusiiache Kigamboni nayo ikawa hivyo. Mwelekeo huo tayari upo. Ndiyo sababu ya uamuzi huo wa Jiji na Wizara ya Ardhi ambao nia yake ni njema, naomba tuwape ushirikiano na msaada unaostahili.
Ndugu Wananchi,
Naomba sasa nimalize kwa kuwakumbusha wenzetu wa Wizara na hasa TEMESA kuhakikisha kuwa kivuko hiki kunatunzwa ipasavyo. Kinafanyiwa matengenezo ya mara kwa mara kwa mujibu wa ratiba yake. Hamzidishi magari, abiria na mizigo kupita uwezo unaostahili. Tukifanya hayo kitadumu na kutuhudumia kwa miaka mingi kama ilivyokusudiwa. Tuukumbuke daima msemo wa Waswahili usemao “Kitunze Kidumu” na Kitunze Kikutunze” Tusifanye kinyume chake.
Baada ya kusema hayo, sasa niko tayari kwa uzinduzi wa kivuko hiki kipya cha Mv. Magogoni.
ASANTENI SANA KWA KUNISIKILIZA
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment