Friday, 1 May 2009

Ajali na Mlipuko wa mabomu Mbagala, Dar

11 wafa kwa mabomu

Watu 11 wakiwamo wanajeshi sita, wamethibitika kufa katika milipuko ya makombora na mabomu iliyotokea juzi katika kambi ya maghala ya silaha ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) Mbagala Kizuiani, Dar es Salaam. Idadi hiyo ya vifo imeongezeka ikilinganishwa na ya juzi, ambapo ilithibitika kuwa watu watatu walikufa katika milipuko hiyo wote wakiwa raia, akiwamo mwanamke mkazi wa Mbagala Kuu eneo la Mwanamtoti aliyekatwa kiuno na chuma cha makombora.

Pamoja na watu hao pia askari sita wengine haijulikani walipo huku wagonjwa zaidi ya 117 wakiwa bado wamelazwa katika hospitali za Temeke na Muhimbili wakiendelea na matibabu na wengine wawili wamelazwa katika Chumba cha Wagonjwa Wanaohitaji Uangalizi Maalumu (ICU).

Rais Jakaya Kikwete jana alitembelea kambi hiyo akifuatana na mawaziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Lawrence Masha, Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Bernard Membe, Naibu Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Emmanuel Nchimbi, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Davis Mwamunyange na wakuu wa usalama akiwamo Mkuu wa Polisi (IGP) Said Mwema.

Akitoa taarifa ya athari ya tukio hilo ambalo bado chanzo chake hakijabainika mbele ya Rais Kikwete, Mkuu wa Tiba wa JWTZ, Profesa Brigedia Jenerali Yadon Kohi, alisema mpaka sasa majeruhi waliohusika katika tukio hilo ni 163 na kati yao 35 wamelazwa wakiwa na majeraha makubwa. “Wagonjwa 24 wamelazwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na kati yao, saba wamejeruhiwa vibaya na watatu wamelazimika kufanyiwa operesheni ya dharura jana (juzi) usiku,” alisema Kohi.

Alisema wagonjwa 11 wamelazwa katika Hospitali ya Temeke huku wengine 117 wakifanyiwa uchunguzi na 11 ndio waliopoteza maisha wakiwamo watano raia na sita askari Jeshi ambao watano wamebainika kufa baada ya kupatikana kwa viungo vyao kama vile vipande vya miguu na nyama vikiwa vimezagaa eneo la tukio na mmoja kufia hospitalini. Alisema kati ya raia watano, wanne kati yao walikufa papo hapo kutokana na athari za milipuko ya mabomu hayo, mmoja ni mtoto aliyekufa kwenye Mto Mzinga alikotumbukia wakati akikimbia kuokoa maisha yake.

Naye Mnadhimu Mkuu wa JWTZ, Luteni Jenerali Abdulrahaman Shimbo, akitoa taarifa ya athari za tukio hilo kwa upande wa Jeshi, alisema milipuko ya mabomu hayo imesababisha hasara kubwa katika maghala hayo ya silaha ambazo hata hivyo idadi na kiasi cha hasara kimetakiwa kisitajwe. Alisema kambi hiyo ambayo ni kiungo cha masuala ya kitaalamu cha Jeshi ilianzishwa mahsusi kwa madhumuni ya kuandaa silaha na zana za kupelekwa Msumbiji na nyingine za dharura.

“Hata askari waliopangiwa kwenda Darfur kama silaha zao zikipatikana na hitilafu huletwa katika kambi hii kuchunguzwa na hupewa nyingine,” alisema Shimbo wakati akitoa mfano wa matumizi halisi ya kambi hiyo. Naye Mkuu wa Kikosi cha Anga, Brigedia Jenerali, F. Olomi, akitoa taarifa ya kambi kwa Rais alisema tukio hilo limesababisha hasara kwa kuharibu kabisa baadhi ya ofisi za kambi hiyo ikiwa ni pamoja na kuteketeza nyumba 50 za raia.

“Hali ilikuwa mbaya, mabomu yalikuwa yanaruka yametekeza ofisi, mashubaka ya kuhifadhia makombora na vifaa vya Jeshi baadhi vimeungua na nyumba 50 za raia zimeteketea kwa moto na nyingine mabati yametoka na kuta kudondoka,” alisema Olomi.

Alisema kazi kubwa kwa Jeshi hilo kwa kushirikiana na vyombo vingine vya Dola, ilikuwa ni kuhakikisha usalama wa raia kutokana na milipuko hiyo ya makombora kusababisha mengine kuruka hadi umbali wa kilometa 21. “Bomu moja aina ya roketi limeokotwa leo (jana) eneo la Banana karibu na Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Julius Nyerere,” alisema.

Pamoja na hayo Olomi alisema bado askari hao hadi jana walikuwa wakiendelea kukagua na kukusanya mabaki ya makombora ambayo hayakulipuka, lakini yaliruka hadi maeneo ya raia na maroketi ambayo yamezagaa katika maeneo mbalimbali ya Mbagala.

Katika ziara hiyo, Rais Kikwete ambaye hakuzungumza chochote zaidi ya kutoa pole kwa wahusika, alitembelea kambi hiyo, baadhi ya maeneo ya wananchi ambayo yameathirika, Hospitali ya Temeke na Muhimbili ambako alizungumza na kuwafariji wagonjwa.

Mganga Mkuu wa Hospitali ya Temeke, Dk. Aisha Mahita, akitoa taarifa yake kwa Rais, alisema wagonjwa 210 walifikishwa hospitalini hapo jana miongoni mwao wakiwamo walioumia vibaya na hadi jana walibaki wagonjwa 39 huku wengine wakiruhusiwa na wengine wakihamishiwa katika hospitali nyingine kutokana na hali zao kuwa mbaya.

Wakati katika Taasisi ya Mifupa (MOI) pekee kwa mujibu wa Ofisa Habari wa Taasisi hiyo, Jumaa Almasi walikuwapo wagonjwa 25, kati yao wanane waliruhusiwa, 13 wamelazwa ambao kati yao wawili wamelazwa ICU.

Katika wodi nyingine ambazo Rais Kikwete alitembelea ikiwamo ya Mwaisela kulikuwa na wagonjwa sita wakiwamo waliovunjika miguu, kiuno na wengine kuishiwa nguvu huku kukiwa na taarifa za kuwapo wagonjwa wengine katika wodi ya Kibasila, lakini idadi yake haikuweza kupatikana mara moja.

Aidha gazeti hili lilitembelea kambi ya Jeshi Kituo cha Mgulani (JKT) ambako kulihifadhiwa watoto na watu wazima 255 waliokimbia milipuko hiyo ya mabomu na hadi jana bado kulikuwa na watu 83 ambao hawajaonana na familia zao kati yao wakiwamo watoto 61 na watu wazima 22.

Aidha kwa uchunguzi uliofanywa na 'HabariLeo' imebainika kuwa baadhi ya wazazi wakazi wa Mbagala jana bado walikuwa wakitafuta watoto na ndugu zao ambapo wengine walifanikiwa kuwaona na wengine bado wanaendelea kuwatafuta.

Hata hivyo kwa tathmini ya haraka iliyofanywa na gazeti hili, hali ya kambi hiyo imeonekana kutulia huku kukiwa hakuna hatari ya kutokea tena kwa milipuko hiyo, ingawa bado kuna hofu kwa baadhi ya wakazi wa eneo hilo ambao walijikusanya wengi barabarani wakati Rais Kikwete alipotembelea eneo hilo.

Kwa upande wake, Kamanda wa Kanda Maalumu Mkoa wa Dar es Salaam, Suleiman Kova, wakati akihojiwa asubuhi na Taasisi ya Taifa ya Utangazaji (TBC) alisema vurugu kubwa na kuumia kwa watu wengi juzi kulitokana udanganyifu na vitisho vilivyokuwa vikisambazwa kwa njia ya simu na baadhi ya watu.

“Watu walizidisha uongo kuliko hali halisi ya tukio, mtu anatuma ujumbe mfupi eti kuna bomu kubwa linasubiriwa likilipuka Dar es Salaam nzima itateketea, jamani kukitokea hali kama hii tulieni msubiri maelekezo kutoka vyombo vya Dola,” alisema. Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM), umetoa salamu za rambirambi na pole kwa wafiwa waliopoteza ndugu zao na kujeruhiwa katika tukio hilo. “Tunaamini tukio hili ni bahati mbaya na kamwe si hujuma.”



source: www.habarileo.co.tz (Imeandikwa na Halima Mlacha; Tarehe: 1st May 2009)

No comments:

Post a Comment