Tuesday, 5 May 2009

Ajali ya mlipuko wa mabomu: Wanajeshi waliopoteza maisha

Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa imewataja wanajeshi watano na ofisa wa jeshi hilo mmoja waliopoteza maisha wakati wakiwa ndani ya ghala la kuhifadhia silaha lililolipuka wiki iliyopita. Wanajeshi hao waliopoteza maisha wakiwa ndani ya ghala hilo wakifanya kazi zao za kawaida na kupoteza maisha ni pamoja na Meja A. M Muhidin, Sajini Amelye Mbeyale, Koplo Phinias Mwambashi, Koplo Mohamed Seif na Koplo Bernard Mbilo. Akizungumza na waandishi wa habari jana, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Hussein Mwinyi alimtaja mwingine aliyepoteza maisha kuwa ni Ofisa Mteule Daraja la Kwanza, Timothy Mtweve ambaye alikwenda eneo la tukio kwa ajili ya kuzima moto na kuwaokoa walioumia katika mlipuko huo.

Alifariki dunia alipofikishwa hospitalini kwa matibabu. Dk. Mwinyi alisema katika tukio hilo, wanajeshi wawili waliokuwa nje ya ghala hilo la kuhifadhia silaha walijeruhiwa. “Wengine mwanajeshi na mpishi walikuwa nje ya ghala walifanikiwa kukimbia baada ya kusikia mlipuko na hao tunawategemea kutusaidia kutoa maelezo ya chanzo cha mlipuko huo,” alisema Dk. Mwinyi.

Dk. Mwinyi alisema kuwa Baraza la Uchunguzi limeshaundwa kuchunguza tukio hilo ambalo lina wajumbe tisa na linaongozwa na Meja Jenerali Sylvester Chacha Rioba. Wajumbe wa baraza hilo ni pamoja na wataalamu wa milipuko, wakemia, maboharia, Ofisa wa Polisi, Ofisa wa Idara ya Zimamoto na Ofisa Mhakiki Mali. Hadidu rejea kwa baraza hilo ni pamoja na kuchunguza na kubaini chanzo, madhara, hasara na kupendekeza hatua za kuchukuliwa ili kuzuia tukio kama hilo lisitokee tena. Sambamba na baraza, hatua za ziada zinachukuliwa kuepusha tukio kama hilo lisitokee katika maghala mengine.

Tahadhari ya usalama inatolewa kwa wananchi wote wasiokote au kuficha chuma chochote kilichotokana na mlipuko, silaha, risasi zilizosambaa eneo la mlipuko na kwenye makazi. Vitu vya aina hiyo vitolewe taarifa kwa timu ya wanajeshi wanaovikusanya au kituo cha Polisi, ni kosa la jinai kama mtu atapatikana anahifadhi silaha, risasi au mlipuko wa aina yoyote”, alisisitiza Waziri huyo.

Waziri huyo alisema kazi ya kusafisha eneo la makazi ya wananchi kwa kuondoa vipande vya mabomu na mabaki ya makombora inaendelea na kuwataka wananchi watoe ushirikiano kwa wanajeshi kuwaonyesha yalipo mabaki. Aprili 29, mwaka huu, ghala lililokuwa limehifadhi silaha ndogondogo, mabomu, makombora na risasi katika kambi ya Jeshi Mbagala lililipuka na kusababisha vifo vya wanajeshi hao na raia 18 sambamba na nyumba kadhaa kuharibika.

Wakati huohuo, serikali imesema kwa mujibu wa tathmini kaya 3,750 za wakazi wa eneo la Mbagala Kuu hazina mahala pa kuishi baada ya nyumba zao kuharibiwa vibaya na milipuko hiyo ya mabomu. Aidha, Sh milioni 660.2 zimechangwa na watu mbalimbali ikiwamo serikali kwa ajili ya kusaidia ununuzi wa chakula, maji, mahema, nguo na mahitaji mengine muhimu.

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kupokea msaada wa Sh milioni 5.2 kutoka kwa Jumuiya ya Mabohora Dar es Salaam, iliyoongozwa na Makamu Mwenyekiti wake, Zainuddin Adamjee, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, William Lukuvi alisema kwa mujibu wa tathmini hiyo mpaka sasa nyumba 4,636 zimeharibika vibaya. “Tunajaribu kufanya kila tunaloweza kuwasaidia waathirika wa tukio hili na tayari serikali imetoa mifuko 3,750 ya mchele ambapo kila kaya itapewa mfuko mmoja wa kilo 30 na maharage kilo 10,” alisema Lukuvi.

Alisema pamoja na hayo wanakabiliwa na changamoto nyingi ikiwamo ya ukosefu wa mahema ambayo mpaka sasa yamepatikana 87 wakati mahitaji halisi ni mahema 550. “Hapa Tanzania hakuna mahala pa kununua mahema hivyo tunategemea kuazima, tumeaongea na Shirika la Umoja wa Mataifa la Wakimbizi (UNHCR) bado tunasubiri,” alisema. Alisema kwa sasa kinachoendelea ni tathmini ambapo timu za wathamini zimeanza kazi lakini zimeongezewa nguvu na wathamini kutoka Morogoro, Pwani na Tanga na wamezungumza na Mkuu wa Chuo cha Ardhi ambaye ameahidi kuongeza wahitimu 20 wa tathmini katika timu hiyo ili kuweza kufanya tathmini ya nyumba lakini pia pamoja na mali.

Akizungumzia wagonjwa, alisema hadi sasa katika Hospitali ya Temeke wapo 12 na wengine 15 wameongezeka jana ambao kati yao tisa wamelazwa, waliokufa ni raia 18 na maiti zote zimetambuliwa ikiwapo iliyoopolewa jana katika mto Mzinga na kati ya maiti hizo 15 zimezikwa Dar es Salaam moja Singida. Kwa upande wa misaada, Lukuvi alisema serikali imetoa Sh milioni 200, Ofisi ya Waziri Mkuu Sh milioni 200, Bakhresa Sh milioni 100, Quality Group milioni 30, Mwenyekiti wa IPP Reginald Mengi Sh milioni 25, Vodacom Sh milioni 20, Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam Sh milioni 20, manispaa zote tatu Ilala, Temeke na Kinondoni Sh milioni 60 na Mabohora Sh milioni 5.2.

Alisema fedha hizo zimetumika kulipia gharama za mazishi, kununulia vyakula, maji, nguo kama vile mablanketi na vyandarua, posho za wathamini, mafuta ya magari na posho za askari Polisi 100 wanaolinda eneo la kambi. Naye Meya wa Manispaa ya Temeke, Jerome Bwanausi, alisema kutokana na malalamiko ya baadhi ya waathirika kwamba misaada haiwafikii mengi ni ya uongo na kwamba timu iliyopangwa kugawa misaada hiyo inagawa kulingana na tathmini inayofanywa na idadi ya kaya. Wakati gazeti hili likiwa eneo la maafa, lilishuhudia kikosi cha askari wa JWTZ kikifukua kifusi cha nyumba zilizobomoka huku kikitoa tahadhari kwa watu kukaa mbali kutokana na kuwapo uwezekano wa mabomu ambayo hayajalipuka



(chanzo: www.habarileo.co.tz,
Imeandikwa na Maulid Ahmed na Halima Mlacha; Tarehe: 5th May 2009 @ 08:48)

No comments:

Post a Comment