Kilimanjaro yafanya kufuru matokeo kidato cha nne
Shule za mkoa wa Kilimanjaro zimeongoza katika
kundi la shule 20 zilizofanya vizuri katika matokeo ya mtihani wa Taifa wa Kidato cha Nne yaliyotangazwa jana na Baraza la Taifa la Mitihani, ambayo mwaka huu ufaulu ni wa asilimia 75.8.
Taarifa ya Baraza hilo iliyotolewa kwa vyombo vya habari jana na kusainiwa na Katibu Mtendaji wake, Dk Joyce Ndalichako, jumla ya watahiniwa 233,848 walifanya mtihani huo Oktoba mwaka na waliofaulu ni 168,420.
Katika kundi la shule 20 bora zenye watahiniwa zaidi ya 35 na chini ya 35, mkoa wa Kilimanjaro umeingiza shule sita, ukifuatiwa na Iringa ambayo imeingiza shule nne Dar es Salaam, Singida, Pwani na Kagera zikiingiza shule mbili kila moja. Wakati Mbeya na Tanga zimeingiza shule moja kila moja.
Dk. Ndaliachako katika taarifa yake kinyume cha miaka ya nyuma ambayo hakufanya mkutano na waandishi wa habari kutoa tangazo hilo muhimu, imezitaja shule kumi bora zenye watahiniwa 35 au zaidi kuwa ni sekondari ya wasichana ya St. Francis ya mkoani Mbeya iliyoshika nafasi ya kwanza Marian Girls ya Pwani nafasi ya pili St. Joseph-Kilocha Seminari ya Iringa nafasi ya tatu Uru Seminari ya Kilimanjaro nafasi ya nne na Seminari ya Dungunyi mkoani Singida nafasi ya tano.
Nyingine ni Sekondari ya Wasichana ya Anwarite ya Kilimanjaro nafasi ya sita St. Mary Goreti ya Kilimanjaro nafasi ya saba Sekondari ya Wavulana ya Feza ya jijini Dar es Salaam nafasi ya nane Seminari ya Don Bosco ya Iringa nafasi ya tisa na sekondari ya Rosmini ya Tanga bafasi kumi.
Taarifa hiyo ilitaja shule kumi bora zenye watahiniwa chini ya 35 kuwa ni sekondari ya Scolastica ya Kilimanjaro iliyoshika nafasi ya kwanza.
Feza Girls ya Dar es Salaam nafsai ya pili
Brookebond ya Iringa nafasi ya tatu Bethelsabas Girls ya Iringa nafsai ya nne Maua Seminari ya Kilimanjaro nafasi ya tano Rubya Seminari ya Kagera nafasi sita St. Mary`s Junior seminari ya Pwani nafasi ya saba Katoke Seminari ya Kagera nafasi ya nane Kilomeni Sekindari nafasi ya tisa na St. Carolus ya Singida nafsai ya kumi.
Taarifa hiyo ilitaja shule kumi za mwisho zenye watahiniwa 35 au zaidi ambazo zimepangwa kuanzia ya kwanza hadi ya mwisho kuwa ni: Selembala ya mkoani Morogoro Kilindi ya Pemba Ngwachani ya Pemba Michiga mkoani Mtwara Ummussalama ya Pwani Chunyu ya Dodoma Busi Dodoma Uondwe pemba Nala ya Dodoma na Maawal ya mkoani Tanga.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo shule kumi za mwisho zenye watahiniwa chini ya 35 ni Juhudi Academy ya Zanzibar, Mima ya Dodoma, Selenge ya Singida, Kijini ya Zanzibar, Kwamkoro ya Tanga, Kwala ya Pwani, Mtende ya Zanzibar, Ng\'oboko ya Shinyanga, Mbuzini ya Pemba na Sekondari ya Ufundi ya Mwadui Shinyanga.
Kati ya waliofaulu wasichana ni 76,472 na wavulana ni 91,948 na waliofeli mitihani hiyo ni 65,428.
Taarifa hiyo inaonyesha kuwa kuna ongezeko la watahiniwa 3,284 waliofaulu mtihani huo ikilinganishwa na idadi ya waliofaulu mwaka jana.
Hata hivyo, taarifa hiyo ilisema kuwa asilimia ya ufaulu inaonyesha kushuka kwa asilimia 10 kutoka asilimia 85.9 ya mwaka juzi hadi asilimia 75 kwa mwaka jana.
Katika ubora wa ufaulu, wavulana wameongoza kwa waliopata daraja la kwanza na kuwaacha wasichana mbali.
Takwimu za Baraza hilo zinaonyesha kuwa wavulana waliopata daraja la kwanza ni 3,743 wakati wasichana ni 1,578.
Katika matokeo ya mwaka 2007 wavulana waliopata daraja la kwanza walikuwa 4,349 wakati wasichana walikuwa 1,900.
Taarifa hiyo ilisema watahiniwa 41,018 waliofanya mtihani wamefaulu katika daraja la kwanza hadi la tatu ikilinganishwa na watahiniwa 44,348 waliopata madaraja hayo mwaka 2007.
Kwa upande wa ubora wa ufaulu katika masomo ya lazima, wavulana wameongoza katika kufaulu wakiwa ni 56,172 ikilinganishwa na wasichana 40,459 waliofaulu.
Katika somo la Hisabati wavulana waliofaulu ni 26,532 kati ya watahiniwa 85,625 wavulana waliofanya mtihani huo, wakati wasichana waliofaulu ni 11,145 kati ya wasichana 69,214 waliofanya mtihani huo.
Kwa upande wa somo la Kingereza wavulana waliofaulu ni 57,122 kati ya wavulana 86,158 waliofanya mtihani huo, wakati wasichana waliofaulu ni 41,314 kati ya wasichana 69,522 waliofanya mtihani huo.
Katika somo la Baiolojia wavulana waliofaulu ni 46,183 kati ya wavulana 85,510 waliofanya mtihani huo, wakati wasichana waliofaulu ni 25,385 kati ya 69,121 waliofanya mtihani huo.
Wavulana wameendelea kuongoza pia katika somo la Kiswahili ambapo waliofaulu somo hilo ni 69,051 kati ya wavulana waliofanya mtihani huo na wasichana waliofaulu ni 57,960 kati ya 69,512 waliofanya mtihani huo.
Kwa upande wa somo la Jiografia wavulana waliofaulu ni 55,449 kati ya wavulana 86,002 waliofanya mtihani huo wakati wasichana waliofaulu ni 36,256 kati ya wasichana 69,505 waliofanya mtihani huo.
Taarifa hiyo ilionyesha kuwa wavulana wameongoza pia katika somo la Civics ambapo waliofaulu walikuwa 56,172 kati ya wavulana 86,112 waliofanya mtihani huo, wakati wasichana waliofaulu ni 40,459 kati ya wasichana 69,527 waliofanya mtihani huo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, ufaulu kwa masomo unaonyesha kuwa watahiniwa wamefanya vizuri zaidi katika somo la Kiswahili ambapo asilimia 81.5 ya watahiniwa wamefaulu.
Ufaulu katika somo la Hisabati uko katika kiwango cha chini ambapo ni asilimia 24.3 tu ya watahiniwa waliofaulu somo hilo.
Baraza hilo limesitisha matokeo ya watahiniwa 5,135 ambao hawajalipa ada ya mtihani na kwamba yatatolewa mara watakapolipa.
Pia limesitisha matokeo ya watahiniwa 495 kutokana na wakuu wa shule husika kutolipa ada ya watahiniwa pungufu ya 35 hadi hapo watakapolipa ada wanayodaiwa.
Baraza hilo pia limefuta matokeo ya watahiniwa 347 kwa kubainika kufanya udanganyifu katika mitihani.
(SOURCE: Nipashe, 2009-02-09 10:10:02 Na Joseph Mwendapole)
Monday, 9 February 2009
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment