Tuesday 12 May 2009

Usitumie pesa kama chambo!

Vitu ambavyo wanawake hupenda mwanamume awe navyo


Sifa moja kubwa kwa wanawake ni ule uwezo wao wa kuzifanyia kwa vitendo hisia zao na mara nyingi huwa wawazi wanapovutiwa au kuchukizwa na kitu lakini huonyesha hisia zao kwa vitendo.

Kwa mfano mwanamume unaweza kukutana na mwanamke na kukubaliana kupeana namba za simu, unapompigia siku nyingine anakubali kutoka na wewe na siku inapowadia mwanamke huyo hatokei, unapompigia anakuambia jambo lingine lililojitokeza. Jambo kama hilo kwa kweli limewatokea wanaume wengi na wameishia kuumia na kuchukia na wengi hata kuwaita wanawake waongo na kwamba hawaaminiki.

Ninachotaka kusema ni kwamba wanawake wengi wanaweza kusema kitu na kufanya kingine na kuona sawa tu kwa vile huwa mara nyingi wanafuata hisia zao. Wanaume wanachotakiwa kufahamu ni kwamba ni mara chache sana wanawake hubadili tabia kama hiyo, hivyo cha kufanya ni wao kujitahidi kuwajengea hisia ili hata wanapopanga miadi ya kuonana, wawe na hisia hizo.

Na hapo ndipo mada yetu inapoanzia ambayo ni kuelezea vitu ambavyo wanawake wanavitaka kwa mwanamume na kuwavutia hisia zao kiasi kwamba mwanamume mwenye sifa hizo anapowekeana nao miadi hawawezi kutohudhuria. Wengi wa wanaume hufikiria kwamba wanawake wengi huvutiwa na wanaume wanaojulikana, matajiri na wenye sura au mwonekano wa kuvutia lakini ukiangalia kiundani hilo linaweza likawa halina ukweli thabiti.

Nasema hivyo kwa kuwa inawezakana kabisa baadhi ya wanawake wakawa hawafahamu ni kitu gani kinachowavutia kwa mwanamume anayemtaka, kwa maneno mengine ni kwamba mambo ya fedha au kujulikana kwa mwanamume kunaweza kutowavutia. Hivyo hata kama mwanamume si tajiri au mwenye sura ya kuvutia anaweza kuwavutia wanawake kulingana na namna atakavyofanikiwa kuzivuta hisia zao.

Jambo la msingi ambalo wanaume wanapaswa kujua kuhusu wanawake ni kwamba wengi wao hutafuta wanaume ambao wanaweza kuzigusa hisia zao bila kujali sura wala fedha walizonazo hayo ni mambo ya nyongeza tu. Japokuwa si wanawake wengi ambao wako tayari kueleza ukweli kuhusu hili, wengi ukiwauliza ni mambo gani wanayatarajia kwa mwenza wao watakwambia kijana mtanashati, mkweli, mwenye mafanikio na mwenye mvuto.

Lakini katika hali halisi kama akifanikiwa kukutana na mwanamume mwenye sifa kama hizo halafu kwa bahati mbaya ikatokea kijana huyo akawa king’ang’anizi ambaye anamfuatafuata mwanamke huyo kila anapokwenda bila kumpa uhuru, basi hawezi kujenga naye uhusiano.

Na kwa upande mwingine mwanamke huyo huyo kama akikutana na mwanamume ambaye hana sifa alizokuwa anazitarajia lakini akafanikiwa kumvuta hisia zake basi anaweza kujenga uhusiano naye tena wa maana. Hivyo basi linapokuja suala la mvuto wa mapenzi kwa mwanamke haliangalii kama mwanamume ni tajiri au masikini, mzuri au anatisha ilimradi tu aweze kuzivuta hisia za mwanamke huyo.

Kinachotakiwa ni mwanamume kujua kutumia lugha na mwili wake pamoja na mbinu nyingine za mawasiliano ambazo zinaweza kumvutia mwanamke badala ya kumkimbia. Si jambo la ajabu siku hizi kwa mwanamume kumpata mwanamke au hata kufanikiwa kuzungumza naye ambaye hapo awali alijiona hatoweza kufanikiwa hilo.

Jaribuni kujiamini na acheni kabisa kutumia fedha kama kigezo cha kumvutia mwanamke kwani wengi wenu fedha zenu zitatumiwa na faida yoyote msiipate. Kumbukeni kuwa anachokitaka mwanamke kwa mwanamume ni tofauti kabisa na kile ambacho kitamvutia kwa mwanamume huyohuyo, hivyo unaweza kuwa na sifa zote lakini kama hukucheza karata zako vizuri ukashindwa kumteka moyo mwanamke unayemtaka.

Dimbwimahaba@dailynews-tsn.com


...............................
chanzo: habari leo Mei 12, 2009.
Imeandikwa na Halima Mlacha; Tarehe: 12th May 2009 @ 07:50

No comments:

Post a Comment