Monday 18 May 2009

Mbagala: wahanga mlipuko wa mabomu

Wapangaji walalamika kubaguliwa


Wakati serikali imesitisha zoezi la kuandikisha nyumba na mali za watu walioathirika kwa mabomu yaliyolipuka katika kambi ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) Mbagala, jijini Dar es Salaam, baadhi ya watu waliokuwa wamepanga katika nyumba hizo wamelalamika kuwa mali zao hazijaorodheshwa kwa ajili ya kufanyiwa tathmini.

Tangu mabomu ya JWTZ yalipolipuka Aprili 29, mwaka huu na kuua raia 20 na wanajeshi sita, nyumba zipatazo 7,241 zimekwishafanyiwa tathmini na Kamati ya Kutathmini Mali za Waathirika, iliyoundwa kufanya kazi hiyo. Watu wapatao 200 walijeruhiwa baada ya milipuko hiyo.

Kamati hiyo iliyoundwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, William Lukuvi, ilitakiwa kutoa ripoti ya awali jana, lakini kutokana na kutokamilika, imeongezewa muda hadi mwishoni mwa mwezi huu.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Cleophace Rweye, alisema kuwa zoezi la kuandikisha nyumba na mali limesitishwa rasmi na jambo wanalofanya sasa ni kumalizia kazi ya kuthaminisha mali hizo.

Rweye alisema zoezi hilo linaendelea vema na wanatarajia kumaliza katika muda waliopewa.

Alisema wanachofanya kwa sasa ni kuandikisha na kuthaminisha nyumba mpya ambazo ziliharibiwa na milipuko ya mabomu iliyotokea Jumatano iliyopita wakati askari wa jeshi hilo walipokuwa wakiteketeza mabomu ambayo hayakuwa yamelipuka katika ajali ya kwanza.

Wakizungumza na Nipashe jana, baadhi ya wenye nyumba na wapangaji walilalamikia zoezi zima la uandikishaji wakidai kuwa mali zao nyingi zilikuwa zimeachwa bila kuandikishwa.

Mchungaji wa Kanisa la African Inland (AIC), Ezekiel Mahalu, alisema wathamini hao wameandikisha kanisa tu na kuacha vifaa vya muziki vilivyoharibika vyenye thamani ya Sh. milioni 10.

Alisema wathamini hao hawakuandikisha mali zozote licha ya kutakiwa kufanya hivyo.

Mpangaji Joshua Kishiwa, alisema wakati Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, alipotembelea Mbagala baada ya milipuko hiyo, aliwaahidi kwamba nyumba na mali zote zilizoharibiwa zitaorodheshwa na kuthaminiwa kwa ajili ya kuwalipa fidia wahusika.

Kishiwa ambaye alidai kuwa mali zake zimeharibiwa kabisa, alisema hakuna hata moja ambayo imeorodheshwa kwa ajili ya kufanyiwa tathmini.

“Wamechukua picha ya mwenye nyumba wangu na kuandikisha nyumba yake, lakini sikuulizwa kuandikisha mali zangu. Nilifikiri kwamba walikuwa wanaanza kwanza kuandikisha nyumba na baadaye kuandikisha mali. Nimeshitushwa sana kusikia kwamba zoezi hilo limefungwa rasmi,” alisema.

Mustapha Muhidin, alisema haikuwa sahihi kwa wathamini kuzingatia tu suala la nyumba kwa sababu katika nyumba waliyokuwa wakiishi kulikuwa na wapangaji watano na hakuna hata mmoja aliyetakiwa kuandikisha mali zake.

Muhidin alihoji kitendo cha wathamini kwenda kinyume cha agizo la Waziri Mkuu kwa sababu mali zao zote zilikuwa zimeharibiwa na sasa hakuna hata mmoja aliyekwenda kuandikisha mali zao.

Aliiomba serikali kufuatilia zoezi zima kwa sababu mwisho wa siku kutakuwa na malalamiko mengi kutoka kwa wapangaji.

Said Mohamed aliwalalamikia wathamini hao kwa kukataa kuandikisha televisheni yake moja, seti ya DVD pamoja na samani. Alisema kwa sasa hana kazi, hali ambayo itamuwia vigumu kupata vitu hivyo katika siku za hivi karibuni.

“Kama zoezi la uandikishaji limefikia mwisho na mali zangu hazijaandikishwa, ina maana kwamba sitaweza kuwa na televisheni tena,” alisema.

Wakati huo huo, Diwani wa Mbagala Kuu, Anderson Chale, alisema walimkamata mtu mmoja akijaribu kuandikisha nyumba yake ambayo ilikuwa katika hatua ya ujenzi.

Alisema mara baada ya kubaini ukweli kwamba mkazi huyo alikuwa na lengo la kuwadanganya wathamini, jina lake liliondolewa katika orodha ya watu wanaotakiwa kulipwa fidia. Alisema serikali itaendelea kutoa chakula kwa waathirika hadi hapo watakapolipwa fidia.


CHANZO: NIPASHE 18th May 2009

1 comment:

  1. Na Mhariri
    19th May 2009b-pepeChapaMaoni
    Juzi Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, William Lukuvi, alitangaza kwamba kamati aliyounda kufanya kazi ya kutathmini uharibifu wa mali za wakazi wa Mbagala ambao nyumba zao zilibomolewa kutokana na mlipuko wa mabomu katika kambi ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Mbagala, ilikuwa imekamilisha kazi yake ya kupitia nyumba zilizoathirika na kilichobakia ni kutathmini hasara iliyopatikana.

    Kwa mujibu wa taarifa za awali nyumba 7,241 zimepitiwa kwa lengo la kufanyiwa tathmini na kazi ya kujua hasa nini kitalipwa itakamilika mwisho wa mwezi huu kamati hiyo itakapokabidhi ripoti yake kwa Mkuu wa Mkoa huo.

    Kama ambavyo tulikwisha kusema huko nyuma, leo tena tunasisitiza kwamba kilichotokea Mbagala ni ajali, lakini pamoja na ajali hii ni jambo jema kwamba serikali ilitoa tamko kwamba kila mwananchi aliyeathirika katika ajali hii ambayo ilisababisha vifo vya watu 26 na wengine zaidi ya 200 kujeruhiwa, ataangaliwa na serikali.

    Kuangaliwa huku kuna maana pana. Kwanza ni kuwapatia msaada wa chakula watu waliopoteza makazi, kuwapatia matibabu kwa gharama za serikali walioumia, lakini kuwafidia waliopoteza nyumba zao ama kwa kubomoka kabisa au kupata hitilafu ambazo zitahitaji gharama kubwa kuzirejesha katika hali yake ya awali.

    Tulipongeza msimamo huu wa serikali, kwa sababu tuliuona kwamba umejaa utu na unakusudia kuwarejesha wakazi wa Mbagala walioathirika na milipuko hiyo iliyoanza Aprili 29, mwaka huu, kwenye utaratibu wa maisha yao ya kawaida kama ilivyokuwa kabla ya janga hilo. Tunaendelea kupongeza tena leo.

    Lakini pamoja na pongezi hizi, mchakato mzima wa kutathmini hasara ya nyumba zilizobomoka tumeelezwa kwamba umewaengua wapangaji wa nyumba husika. Kwa maana kwamba kilicholengwa ni kutoa fidia ya nyumba iliyobomoka.

    Sote tunajua Dar es Salaam si kila anayeishi katika nyumba ni mmiliki wake. Wapo watu wengi pengine ndio wengi kuliko wote ambao wamepanga nyumba za watu. Hawa huishi katika nyumba hizi kwa kulipa kodi ya pango tu kwa ajili ya nyumba ya mwenye mali, lakini vitu vingine vyote katika nyumba hizo, yaani samani na vifaa vingine ni mali ya wapangaji.

    Hawa kwa vyovyote vile katika ajali hii wamepoteza mali; samani za ndani, nguo zao, vyakula vyao lakini na vitu vingine vyenye thamani kubwa. Hawa ni waathirika pengine kuliko mwenye nyumba ambaye wala haishi kwenye nyumba iliyobomolewa.

    Wapangaji hawa ndio waathirika halisi, wameumia, wamepata matatizo ya kisaikolojia, lakini la muhimu zaidi ndio wanajua maana hasa ya milipuko hii. Hawa wameumia kwa kila hali, lakini ni jambo la kusikitisha kusikia kwamba eti serikali haijawafikiria katika mchakato mzima wa kutoa fidia.

    Tunasema kama kweli kundi hili ambalo ndilo limeathirika zaidi, yaani wapangaji wa nyumba zilizobomoka, halimo kwenye mchakato wa walengwa wa fidia, basi kuna kasoro kubwa katika zoezi zima la tathmini ya fidia.

    Ni katika kutambua hali hii, sisi tumeguswa na kwa kweli tunaiomba serikali, hususan Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, ajaribu kufikiria kilio cha wapangaji hawa kwa sababu kama wenye nyumba wameathirika kwa kupoteza mali, wapangaji ni zaidi kwani licha ya kupoteza mali zinazohamishika, pia wameathirika wenyewe miili yao kwa majeraha na kisaikolojia.

    Hatua yoyote ya kuwalipa fidia wenye nyumba bila kuwakumbuka wapangaji, ni utaratibu wa kubagua waathirika wa mabomu, haufai na haustahili kuungwa mkono hata kidogo.

    Kila tukitazama hali ya mambo inavyokwenda Mbagala, tunazidi kuamini kwamba suala hili ni moja ya mitihani mikubwa na migumu ya Lukuvi katika nafasi yake ya kiasiasa.

    Tunasema ni mtihani kwa sababu hatuoni ni jinsi gani wapangaji hawa watakaa kimya huku haki zao zikikanyagwa hivi hivi tu. Tunamshauri Mkuu wa Mkoa atafakari suala hili kwa makini na kuchukua hatua haraka ili kuepuka mgogoro usio na faida kwake mbele ya safari.




    CHANZO: NIPASHE Na mhariri

    ReplyDelete