Thursday 18 June 2009

'Kila Mtanzania ana haki ya kumiliki ardhi'

Watakaouza ardhi kwa wageni kushitakiwa

Serikali itawashitaki wananchi watakaouza ardhi kwa wageni sanjari na wataonunua, na itaichukua ardhi hiyo.

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, John Chiligati amesema leo bungeni mjini Dodoma kuwa, kuuza ardhi kwa raia wa kigeni ni kuvunja sheria hivyo anayeuza na anayenunua wanatenda kosa.

Waziri Chiligati amewaeleza wabunge katika kikao cha nane, mkutano wa 16 wa Bunge kuwa, ardhi ni mali ya umma chini ya Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.

“Sheria imesema, raia wa nje hawezi kumiliki ardhi hapa Tanzania isipokuwa mwekezaji” amesema Chiligati.

Amesema, kila Mtanzania ana haki ya kumiliki ardhi bila kubaguliwa, lakini wageni wanaoruhusiwa kufanya hivyo ni wawekezaji tu wenye vibali kutoka Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) na kwa kuzingatia Sheria ya Uwekezaji namba 26 ya mwaka 1997.

Chiligati amesema, Mtanzania anayeishi mjini ana haki ya kumilikishwa ardhi aitumie kwa miaka 33, 66 hadi 99, na kwamba vijijini haki ya kuitumi ardhi haina ukomo.

Wakati akijibu swali la Mbunge wa Kongwa, Job Ndugai, Chiligati alisema, katika bajeti ya Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2009/2010 Serikali imetenga fedha za kupima mipaka ya vijiji vyote nchini ikiwa ni sehemu ya mchakato wa kuwamilisha wananchi ardhi.

Amesema, baada ya mashamba ya wananchi kupimwa, wao wataamua namna ya kuyatumia.

Wakati akijibu swali la Mbunge wa Bariadi Magharibi, John Cheyo, Chiligati alisema, maeneo yanayomilikiwa kimila mkoani Kilimanjaro maarufu kwa jina la vihamba pia yatapimwa ili yapate hati miliki.

Amesema, zitatolewa hati kwa kihamba kimoja kimoja, na kama kuna vihamba vingi vinavyomilikiwa na ukoo, itatolewa hati moja kwa vihamba hivyo na atakabidhiwa mkuu wa ukoo husika.

“Sheria zetu za ardhi haziruhusu wageni kumilikishwa ardhi”amesema Chiligati wakati akijibu swali la Mbunge wa Gando, Khalifa Suleiman Khalifa.

Kwa mujibu wa Waziri Chiligati, hadi sasa jumla ya wageni 20 wamemilikishwa jumla ya hekta 69,128 kwa ajili ya uwekezaji kwenye kilimo, Viwanda na hoteli.

Amesema, wageni 15 kati ya hao wamemilikishwa ardhi kati ya mwaka 2005 na mwaka jana, na kwamba Serikali imepata sh milioni 711.2 kupitia vyanzo mbalimbali vya taratibu za kuwamilikisha ikiwamokodi ya pango la ardhi na hati.

“Baada ya mwaka 2001 kama kuna mgeni ameuziwa ardhi chini ya utaratibu huu ni kinyume cha sheria” amesema Chiligati.



chanzo: habari-leo, Imeandikwa na Basil Msongo, Dodoma; Tarehe: 18th June 2009 @ 14:02

No comments:

Post a Comment