Thursday 16 April 2009

Waziri Mkuu azungumzia kero za wananchi

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda amesema shughuli za Kampuni ya DECI (Development Enterprenueurship Community Initiative) za wanachama kuweka fedha kupata faida marudufu ni sawa na upatu na ni kinyume cha sheria za nchi.

Akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari ofisini kwake jijini Dar es Salaam leo (Jumanne Apr. 14, 2009) alisema ndiyo maana Serikali imeunda timu ya kuingalia DECI na kuchukua hatua bila kuwaathiri wanachama wa DECI.

“Hakuna cha maono wala ufunuo, DECI ni upatu tu. DECI siyo mkombozi ni ujanja ujanja ambao ambao lazima utaleta matatizo hatimaye,” alisema.

Shughuli za upatu ni kinyume cha sheria Na. 8 ya mwaka 2006, iliyoidhinishwa na Rais Januari 5, mwaka 2007, kuwa ni kosa kuendesha shughuli za upatu ambao hauna usalama wa fedha watu wazochanga, aliongeza.

Alisema kuwa timu iliyoundwa na serikali kuangalia shughuli za DECI ina wataalamu kutoka Benki Kuu, Wakala wa Soko la Mitaji na Dhamana (Capital Markets Authority) na Idara ya Polisi.

DECI ilianza shughuli zake nchini mwaka 2007 na iliandikishwa kwa Wakala wa Usajili wa Makampuni (BRELA).

Waziri Mkuu alisema DECI ilianzishwa kama chama cha kuweka na kukopa, lakini baadaye ikawa inaendesha upatu na kwamba ina wanachama zaidi ya 430,000 na ina ofisi 46 katika mikoa 18 kati ya 26 nchini, kwa mujibu wa taarifa alizopata.

Benki ina akiba ya Sh. bilioni 1, lakini fedha ambazo zimezungushwa kupitia DECI ni Sh. bilioni 13 ambazo zilitolewa na kuchukuliwa na wanachama kama faida.

Kuhusu suala la ardhi katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, Waziri Mkuu alisema kuwa suala la ardhi linatawaliwa na sheria za kila nchi na siyo la ushirikiano katika jumuiya.

Alisema suala ardhi, kama vile la hoja ya mtu akiikaa katika nchi moja kwa mfululizo kwa miaka mitano apate uraia wa nchi hiyo, ni masuala ambayo hayawezi yakachukuliwa kwa pupa na Tanzania lazima iyaangalie kwa makini.

Kuhusu udahili wa wanafunzi wa vyuo vikuu vya umma ambavyo baadhi yao vilifungwa kwa muda kutokana na suala la uchangiaji, Waziri Mkuu alisema udahili umekwenda vizuri na kunavigezo vipya vya kujua uwezo wa mwanafunzo kucjangia kiasi gani.

Waziri Mkuu pia alisema Tanzania isisite kuhusu kuwaruhusu wakulima wakubwa binafsi kuwekeza katika kilimo cha kisasa cha kibiashara kwani bado kuna ardhi kubwa yenye rutuba lakini haijaguswa.

Alisema kinachotakiwa ni kuwa na Benki ya Ardhi ili muwekezaji akitaka kuwekeza katika kilimo anapewa ardhi ambayo kwa mfumo wa Tanzania ni ya Serikali na inatolewa kwa kukodishwa kwa masharti maalum
.

Kuhusu uvunjifu wa amani huko Tarime na maeneo mengine katika mkoa wa Mara, Waziri Mkuu alisema Serikali imepanga kuwa na mkoa wa kipolisi wilayani Tarime ili kuimarisha ulinzi.

Vilevile, inafaa kutenga eneo la amani la watu kuweza kukimbilia kama vile kuwa na kambi ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) katika maeneo yenye magomvi.

Kuhusu maagizo ya Waziri Mkuu kwa Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuangalia hesabu za Kituo cha Mabasi cha Ubungo na Soko la Kariakoo, Waziri Mkuu alisema kazi hiyo imekwishaanza na kwamba amepewa muda wa kutosha kuikamilisha.
(mwisho)

Imetolewa na:
Ofisi ya Waziri Mkuu
S.L.P. 3021
DAR ES SALAAM


source: lukwangule blog (Beda Msimbe)

No comments:

Post a Comment