Monday 16 March 2009

Lawama: utoaji wa hatimiliki za viwanja TZ

Ufisadi watikisa Ardhi

Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi imetupiwa tuhuma nzito za ufisadi katika suala zima la utoaji wa hatimiliki za viwanja.

Tuhuma hizo zimetolewa na wananchi mbalimbali ambao wanadai kwa muda mrefu sasa wamekuwa wakihangaikia bila ya mafanikio kupata hati za miliki za viwanja vyao ambazo hutolewa na wizara hiyo.

Wizara hiyo inalaumiwa kuwa na urasimu mkubwa katika utoaji wa hati hizo kiasi cha kusababisha waombaji wakae muda mrefu bila ya kuzipata na wakati mwingine kulazimika kutoa rushwa kwa baadhi ya maafisa wake wasio waaminifu ili waweze kuzipata kirahisi.

Wakizungumza na Nipashe Jumapili kwa nyakati tofauti kuhusiana na suala hilo, baadhi ya wananchi wameilalamikia Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi, kuwa imekuwa ikiwazungusha kwa muda mrefu katika kuwapatia hati za viwanja vyao pamoja na kwamba wamekamilisha taratibu zote zinazotakiwa.

Wananchi hao wamelalamika kuwa kutokana na kucheleshwa kupata hati hizo kwa sababu zisizojulikana, wamekwama kufanya shughuli zao mbalimbali za maendeleo zinazohusiana na viwanja hivyo kama vile kuviendeleza au kutumia hati hizo kuomba mikopo benki kwa ajili ya kupambana na umasikini.

Mmoja wa wananchi hao kutoka mkoani Arusha ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini, alidai amekuwa akizungushwa kwa muda wa miezi mitano sasa kupata hati ya shamba lake, hali ambayo alidai imekwamisha mipango yake mingi ya kukiendeleza kiwanja hicho pamoja na kuitumia hati hiyo kuomba mkopo benki.

Alisema yeye ni mmoja wa watu waliohamasika na mpango wa serikali wa kuwapatia wananchi hati miliki za maeneo yao baada ya kuyapima ili waweze kuomba mikopo benki kwa ajili ya kupambana na umasikini, lakini Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi inamkatisha tamaa kutokana na utaratibu wake usioeleweka wa kutoa hati hizo.

``Serikali inatuhamasisha wananchi kupima maeneo yetu ili tupewe hati za umiliki zitakazotuwezesha kukopa benki, sasa tunashangazwa na wizara hii ambayo ndiyo yenye jukumu la kutoa hati hizo kutuzungusha kwa muda mrefu na wala hatujui tatizo ni nini maana hatujibiwi chochote,`` alisema.

Alifafanua kuwa yeye pamoja na wenzake wengine ambao nao wanakabiliwa na tatizo kama hilo, wametimiza taratibu zote za kupatiwa hati hizo kuanzia ngazi ya kijiji hadi kanda ambako ndiko hati hizo inakotolewa, lakini wameelezwa kuwa kanda haina mamlaka ya kuzitoa na kwamba zimetumwa wizarani Dar es Salaam ambako zimekwama huko wao wakisubiri kwa muda mrefu bila ya wao kujua kinachoendelea.

``Kwa utaratibu mtu anatakiwa kuanzia ngazi ya kijiji kwa kuitisha mkutano wa wanakijijiji wakikubali unaenda wilayani ambako unapewa kibali cha kupima ardhi kabla ya kwenda ngazi ya mkoa na kisha kanda ambako hati husajiliwa na kutiwa saini, mimi nimetimiza yote hayo lakini nilipoenda ofisi ya kanda nikaambiwa zimepelekwa wizarani ambako zimekwama,`` alieleza.

Nipashe Jumapili lilipowasilliana kwa njia ya simu na Kamishna wa Ardhi Kanda ya Kaskazini ili kujua ni tatizo gani linalosababisha kuchelewa kutolewa kwa hati hizo kufuatia malalamiko ya baadhi ya wananchi alikataa kutoa ushirikiano na badala yake ilitaka wizara ndiyo iulizwe kuhusiana na suala hilo.

Malalamiko kama hayo pia yametolewa na baadhi ya wananchi jijini Dar es Salaam na kutoka mikoa mingine, kuwa inawachukuwa muda mrefu sana kupata hati za umiliki wa maeneo yao huku wakiwa hawajui tatizo ni nini pamoja na kufuata taratibu zote zinazotakiwa.

Wananchi hao wamemuomba Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi, John Chiligati, kulifuatilia kwa karibu tatizo hilo ili kulipatia ufumbuzi wa haraka, kwa kile walichodai kuwa baadhi ya maafisa wa wizara hiyo siyo waaminifu kwani wamekuwa wakifanya makusudi kuchelewesha kutoa hati ili waweze kupewa rushwa.

Walisema wizara hiyo inatakiwa kwenda sambamba na kauli mbiu ya Rais Jakaya Kikwete ya Ari Mpya, Nguvu Mpya na Kasi mpya katika utendaji wake ikiwa ni pamoja na kuwaondoa watumishi wote wanaokwenda kinyume na maadili ya kazi zao ili kuleta ufanisi.

Nipashe Jumapili lilipowasiliana na Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi, John Chiligati, kuhusiana na malalamiko hayo ya wananchi alionekana kushangazwa na maelezo hayo, akieleza kuwa kwa sasa hakuna tatizo kama hilo la ucheleweshaji wa utoaji wa hati za umiliki wa ardhi.

Alieleza kuwa tatizo hilo lilikuwapo zamani lakini wizara yake imeshalifanyia kazi na kwamba kwa sasa halipo tena, tofauti na madai ya wananchi hao.

Chiligati, alifafanua kuwa kutokana na tatizo hilo kuwa sugu siku za nyuma, wizara yake ilianzisha utaratibu wa maombi ya hati za umiliki wa ardhi kushughulikiwa katika kanda badala ya wizarani, ili kuwawezesha wananchi kuzipata bila ya usumbufu na kwa haraka.

``Tatizo hilo limekuwa historia, tangu tupate uhuru maombi yote yalikuwa yanashughulikiwa wizarani tu na Kamishana wa Ardhi, lakini sasa tumeunda kanda tano kwa ajili ya kurahisisha mambo, mimi ndiyo muasisi wa utaratibu huu, wananchi wanatakiwa kupeleka maombi yao huko kwa ajili ya kupatiwa hati za umiliki wa ardhi badala ya kuja moja kwa moja wizarani kama zamani,`` alifafanua.

Alizitaka kanda hizo kuwa ni Kanda ya Kaskazini, Kanda ya Ziwa, Kanda ya Kusini, Kanda ya Kati na Kanda ya Mashariki.

Alitoa wito kwa mwananchi yoyote anayezungushwa kupata hati hizo baada ya kukamilisha taratibu zote aende wizarani akaonane naye ili aweze kushughulikia tatizo hilo.

Kwa muda mrefu sasa kumekuwa na malalamiko mengi kutoka wananchi wakiilalamikia baadhi ya maofisa wa Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi kuwa wamekuwa kikwazo katika utoaji wa hati za umiliki wa ardhi kwa lengo la kupewa rushwa, hali ambayo inakwamisha mipango yao ya kuboresha hali zao za maisha.


SOURCE: Nipashe, 2009-03-15 14:08:05
Na Abdallah Bawazir

No comments:

Post a Comment