Monday 16 February 2009

Uwanja Mpya wa Taifa uko tayari sasa

JK akabidhiwa Uwanja

Rais wa Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China, Hu Jintao jana alizindua na kukabidhi Uwanja mpya wa Taifa ulioko, jijini, Dar es Salaam kwa serikali ya Tanzania.

Rais Jintao alikabidhi uwanja huo kwa Rais Jakaya Kikwete katika shughuli iliyofanyika uwanjani hapo kuanzia saa tisa alasiri.

Uzinduzi huo, ambao pia ulifanywa kwa pamoja na Rais Kikwete na kushuhudiwa na viongozi mbalimbali akiwemo Rais Mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa, ulifanyika jijini Dar es Salaam jana.

Rais Jintao alisema ujenzi wa uwanja huo, ni kiashiria cha ushirikiano mkubwa uliopo kati ya serikali ya China na Tanzania na kwamba nchi yake imekuwa ikifadhili miradi mbalimbali ikiwemo ya sekta za uchumi, afya na miundombinu.

Akimkaribisha Rais Jintao kuzungumza na hadhara hiyo, Rais Kikwete, ambaye alizungumza kwa lugha mbili za Kiingereza na Kiswahili, aliishukuru Serikali ya China kwa msaada huo.

Alisema kuwa ujenzi wa uwanja huo ulifuatia ombi lililotolewa na Rais Mstaafu Mkapa, kwa Rais Jintao mwaka 1998 wakati alipofanya ziara nchini humo.

Alisema yeye ndiye aliyesaini mkataba huo wakati huo alikuwa ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na leo hii ndiye aliyefungua kwa pamoja na Rais Jintao.

Alisema uwanja huo ni kumbukumbu nzuri ya kihistoria ya ushirikiano kati ya Serikali ya Jamuhuri ya Watu wa China na Tanzania.

Hafla hiyo ya takribani saa mbili ilipambwa na vikundi vya ngoma za kitamaduni, bendi ya muziki na nyimbo za kichina ambapo Rais Jintao na Rais Kikwete mara baada ya kumaliza kuzindua uwanja huo walipeana mikono na baadhi ya wasanii.

Mbali na hafla hiyo kushuhudiwa na Rais Mstaafu Mkapa, wengine walioshuhudia ni Waziri Mstaafu wa awamu ya Tatu, Fredrick Sumaye, mawaziri na viongozi wengine wa Serikali na chama.

Uwanja huo ulianza kujengwa mwaka 2005 una uwezo wa kuingiza watu wapatao 60,000, una vikolombwezo kibao vikiwamo televisheni kubwa, chumba cha kinachoweza kutumika ofisi ya Rais na vyoo vipatavyo 3000.


SOURCE: Nipashe 2009-02-16 10:04:36
By Sharon Sauwa

No comments:

Post a Comment